0

Dk Slaa atarajiwa kuchukua fomu kugombea

Fomu za ubunge, udiwani mwisho kutolewa

kesho

Celina Mathew

WAKATI makada wa vyama vya NCCR-

Mageuzi na CUF wakiwa wametangaza

kugombea urais, Chama cha Demokrasia na

Maendeleo (Chadema), kimeanza mchakato

wa kumpata mgombea wake wa nafasi hiyo.

Chama cha NCCR-Mageuzi tayari

kimemtangaza Dk. Joseph Kahangwa kuwa

mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa

Tanzania huku Chama cha Wananchi (CUF)

Profesa Ibrahim Lipumba akijitokeza kuwania

kiti hicho kwa mara ya tano.

Kutokana na hali hiyo, Chadema kimesema

mchakato wa uchukuaji na urejeshaji wa

fomu kwa wagombea urais unaanza Julai 20

hadi 25, mwaka huu, na uchukuaji na

urejeshaji fomu za ubunge ulianza Mei 18

hadi Juni 25, mwaka huu.

Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene

aliliambia gazeti hili Dar es Salaam jana

kuwa uchukuaji wa fomu hizo za ubunge

unalenga majimbo ambayo chama hakina

wabunge kwa sasa, pamoja na fomu za

ubunge wa viti maalumu.

Makene alisema mchakato wa uchukuaji na

urudishaji fomu kwa ngazi ya ubunge na

udiwani unaendelea vizuri na kwamba

mwisho wa wagombea kuchukua na

kurudisha fomu hizo ni kesho na baadaye

michakato mingine itafuata.

Alisema kwa sasa hana majina ya wabunge

au madiwani waliorejesha fomu kwa sababu

mchakato huo unafanyika nchi nzima.

Alisema wabunge wanarudisha katika

majimbo yao na madiwani katika kata zao.

Hata hivyo, taarifa kutoka ndani ya chama

hicho zinaeleza kuwa huenda Katibu Mkuu

wa chama hicho, Dk. Willbrod Slaa

akagombea nafasi hiyo na ndiye anayepewa

nafasi kubwa.

Katika uchaguzi wa mwaka 2010, Dk. Slaa

alipeperusha vyema bendera ya chama hicho

katika uchaguzi wa rais baada ya kuibuka

mshindi wa pili nyuma ya Rais Jakaya

Kikwete.

Mwaka 2005, Mwenyekiti wa chama hicho

taifa, Freeman Mbowe aligombea kiti cha

urais na kwamba mwaka huu, mwenyekiti

huyo hajaweka bayana kama atarejea

kugombea ubunge katika Jimbo lake la Hai

mkoani Kilimanjaro.

Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Salum

Mwalimu ameshachukua fomu za kuwania

ubunge Jimbo la Mkwajuni Zanzibar. Jimbo

hilo ndilo pekee ambalo liliachwa kwa

Chadema baada ya majimbo mengine

kuachiwa CUF chini ya Umoja wa Katiba ya

Wananchi (Ukawa).

Ukawa unaunganisha vyama vya upinzani vya

Chadema, CUF, NCCR Mageuzi na NLD,

vimepanga kusimamisha mgombea mmoja

wa urais katika uchaguzi wa mwaka huu, na

kwamba baada ya kila chama kumpata

mgombea wake watakaa kumchagua mmoja

kati yao kupeperusha bendera ya upinzani.

Tayari Chama Cha Mpinduzi (CCM),

kimeanza mchakato wa kumpata mgombea

wake wa urais kwa makada wake kuchukua

fomu kutafuta saini za wadhamini 450

kutoka mikoa 15. Mpaka sasa makada

ambao wamejitokeza kuchukua fomu ni 40.

Post a Comment

 
Top