0

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), leo kinazindua
operesheni mpya ya kuwaandaa wanawake
kufanya “maamuzi magumu” kwenye
Uchaguzi Mkuu ujao.
Kwa sasa, chama hicho kikuu cha upinzani,
kinaendelea na kampeni ya “Amsha
Amsha”, ambayo inalenga kuhamasisha
wananchi kujitokeza kujiandikisha kwenye
Daftari la Wapigakura.
Jana, Chadema ilitoa taarifa inayoeleza
kuwa sambamba na kampeni hiyo ya
Amsha, Amsha”, chama hicho kinaanza
operesheni mpya itakayozinduliwa na
katibu wake mkuu, Dk Willibrod Slaa huku
wanamuziki nyota, Christian Bella, Profesa
Jay na Flora Mbasha wakipamba uzinduzi
huo.
Mratibu wa operesheni hiyo, Lilian Wasira
alisema jana kuwa shughuli hiyo itafanyika
kwenye viwanja vya Tanganyika Packers,
Kawe jijini Dar es Salaam.
“Maandalizi yamekamilika, wanawake Dar
es Salaam na Pwani waje wajengeke kifikra
ili kufanya maamuzi magumu katika
uchaguzi unaokuja,” alisema Wasira.
Alisema operesheni hiyo itafanyika nchi
nzima kuhamasisha wanawake
kujiandikisha kwenye Daftari ya
Wapigakura na kuwapa elimu ili watambue
nafasi yao katika jamii na uwezo wao
kuleta maendeleo ya kweli,” alisema
Wasira.
Kada huyo, aliyewania uenyekiti wa Baraza
la Wanawake wa Chadema bila mafanikio,
alisema: “Zama za wanawake kupewa
khanga, vitenge, vilemba na kofia wakati
wa uchaguzi zimepitwa na wakati, lazima
wajithamini, ndiyo maana tumeanzisha hii
operesheni ili tuwajenge kiuwezo.”
Alisema ni wakati mwafaka kuachana na
fikra za kurubuniwa na kuuza haki zao za
msingi kwa rushwa za aina mbalimbali
kama “chumvi”, akishauri watambue kuwa
njia pekee ya kuiondoa CCM madarakani ni
kujiandikisha katika Daftari la Wapigakura
na kugombea uongozi.
“Hatutaki kuona hali ikiendelea. Saa ya
ukombozi imefika, mwanamke amekuwa ni
mwathirika wa matatizo mbalimbali
kwenye jamii, hivyo asiache kuja kesho
(leo) ili Tanzania izaliwe upya Oktoba,”
alisema Wasira.
Mbali na Dk Slaa, hafla hiyo itahudhuriwa
na mbunge wa Kawe, Halima Mdee na
wasanii wa muziki, wote wakiwa na lengo
la kutoa hamasa kwa wanawake nchini
kushiriki katika siasa. Ikiwa ni miezi minne
imesalia kabla ya uchaguzi wa Oktoba,
Chadema imesambaza makada wake walio
kwenye mabaraza ya wanawake na vijana
kwenda maeneo mbalimbali kuhamasisha
uandikishaji wapiga kura.
Juzi gazeti hili lilimkariri mkurugenzi wa
mafunzo na uchaguzi wa Chadema, Benson
Kigaila akisema kwa sasa wanaelekeza
nguvu katika uandikishaji wa wapigakura
ili kutengeneza mazingira mazuri ya
ushindi.
Hamasa hiyo inakwenda sambamba na
mchakato wa kuchukua na kurudisha fomu,
ikiwa ni siku saba kabla ya siku ya mwisho
ya hatua hiyo kwa watiania wa ubunge na
udiwani katika maeneo yasiyo na
uwakilishi wa madiwani na wabunge.

Post a Comment

 
Top