0
 
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Francis Nanai akichangia wakati wa mkutano wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (Moat) na wahariri jijini Dar es Salaam juzi. Mkutano huo ulikuwa ukijadili Muswada wa Sheria ya Vyombo vya Habari. kulia ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Azam TV, Tido Mhando. Picha na Venance Nestory. 

Serikali inakusudia kuwasilisha bungeni, miswada miwili ya Haki ya Kupata Habari na ule wa Huduma za Vyombo vya Habari ili iweze kupitishwa kuwa sheria.
Wadau wa habari, ambao wamekuwa wakipigania kupata sheria itakayowapa uhuru wa kukusanya, kuandika na kusambaza habari kwa kuzingatia maslahi ya taifa, watafurahi kuona rais wao anasaini, kuwa sheria, miswada yenye maudhui rafiki, lakini si kama ilivyo kwa miswada hii miwili.
Harakati za wadau wa habari zilianza katikati ya miaka ya 1990, kupigania chombo huru cha kusimamia wanahabari ambacho ni Baraza la Habari Tanzania (MCT) na itungwe sheria mpya itakayotoa uhuru wa habari.
Baadaye walijikusanya na kuandaa miswada miwili; mmoja ni wa Haki ya Kupata Habari na wa pili ni wa Huduma za Vyombo vya Habari na wakawasilisha serikalini. Serikali ilipokea miswada hiyo na iliahidi kuiwasilisha bungeni, kwa mara ya kwanza mwaka 2007.
Hata hivyo, haikuwasilisha miswada hiyo, badala yake ilianza kuhangaika kutunga vipengele vya marekebisho ya sheria ya magazeti ya mwaka 1976 na sheria ya utangazaji ya mwaka 1993 kuongeza vifungo, faini ya mamilioni ya shilingi na kesi zilizofunguliwa dhidi ya mwanahabari aliyeshitakiwa kwa kuandika habari za kashfa ziharakishwe kusikilizwa. Wabunge walikataa marekebisho hayo wakataka
Serikali iwasilishe sheria nzima kama ilivyokubaliwa na wadau wa habari.
Katika namna inayoshangaza, baada ya danadana za muda mrefu, Serikali iliwasilisha miswada hiyo katika Bunge la Februari ijadiliwe, chini ya hati ya dharura. Wadau wa habari walijiuliza, kwa nini Serikali iwasilishe miswada hiyo kwa dharura? Kwa nini iwasilishe miswada hiyo bila kuwapa wadau fursa ya kujadili maudhui yake? Je, Serikali inaogopa nini kukutana na wadau wa habari kujadili miswada hiyo?
Kumbe Serikali iliingiza vipengele ambavyo si rafiki kwa wadau wa habari kwani badala ya kukuza uhuru na maadili ya habari vinakandamiza uhuru na kupora haki yao kama ilivyoainishwa katika Ibara ya 18 ya Katiba.
Katika miswada hiyo, imependekezwa: Kiwango cha elimu kwa mwanahabari kiwe shahada ya kwanza; mtu haruhusiwi kumiliki vyombo vingi vya habari; mwandishi atakayepatikana na kosa faini Sh20 milioni au kifungo kisichopungua miaka mitano au adhabu zote mbili kwa pamoja kwa mshitakiwa atakayethibitishwa na mahakama kutenda kosa.
Vilevile, imependekezwa vyombo vya habari vya binafsi kutakiwa kujiunga na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) saa 2.00 usiku kila siku kwa ajili ya taarifa ya habari. Vipengele hivi ni vizito na havifai.
Ni jambo zuri kwa mwanahabari kuwa na elimu nzuri ili aweze kuwa na umilisi wa kazi yake ya kuhabarisha na kuelimisha jamii, lakini tunajiuliza kwa nini sharti la elimu ya juu liwe kwa wanahabari tu na siyo kwa walimu, mahakimu, na viongozi? Kwa nini Serikali inatunga sheria kuvibana vyombo vya habari vya hapa nchini na siyo vya kimataifa?
Kwa nini mkazo wa adhabu usiwe kwa mafisadi, wabadhirifu wa mali ya umma badala yake Serikali imewalenga wanahabari? Kwa nini Serikali imevizia dakika za mwisho na kuanzisha mgogoro na wadau wa habari tena kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu?
Tunawaomba wabunge, wapitie miswada hiyo kwa umakini, waisome na kukataa vipengele vyote ambavyo havitoi afya njema kwa tasnia ya habari. Wanahabari wanahitaji uhuru na jamii inataka uhuru kwa kusoma na kusikia habari wanazotaka kutoka vyombo binafsi bila kulazimishwa kwa sheria.

Post a Comment

 
Top