Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linawashikilia watu sita (6)
kwa makosa mbalimbali yakiwemo ya kumiliki silaha kinyume cha sheria,
kulima na kukutwa na bangi pamoja na kuingia nchini bila kibali,
kufuatia operesheni inayoendelea Mkoani Dodoma kusaka watuwanaojihusisha
na uhalifu wa aina mbalimbali.
Akithibitisha matukio hayo kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi DAVID MISIME - SACP amewataja
watu wanaoshikiliwa na Polisi kuwa ni ERASTO DIHELELA mwenye miaka 31,
mkulima, mkazi wa kijiji cha Lukole aliyekamatwa na silaha aina ya
Gobore isiyokuwa na namba pamoja na Golori zake 11 na vipande 17 vya
nondo akilimiliki bila kuwa na kibali. Mtuhumiwa huyo pia alikutwa
amelima bhangi kwa kuchanganya na mahindi katika shamba lake la hekari
moja.
Mtu wa pili ni HAPPY GIBSON mwenye miaka 28, mkulima, mkazi
wa Kijiji cha Lukole akiwa na silaha aina ya Gobole nyumbani kwake bila
kuwa na kibali cha kumiliki silaha hiyo. Vile vile katika kupekuliwa
nyumbani kwake mtuhumiwa huyu alikutwa na bhangi kilo tano (5)
alizohifadhi ndani ya nyumba yake tayari kwa kusafirisha.
Kamanda MISIME amesema katika oparesheni hiyo pia
amekamatwa HAMISI MWIKOLA mwenye miaka 28, mkulima, mkazi wa Kijiji cha
Lukole akiwa amelima bhangi kwa kuchanganya ndani ya shamba lake la
mahindi hekari mbili.
Watuhumiwa hawa wote wamekamatwa siku ya tarehe 21/03/2015
katika kitongoji cha shuleni mlimani kijiji cha Lukole kata ya Kingiti
tarafa ya Kibakwe Wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma na watafikishwa
mahakamani mara baada ya taratibu kukamilika.
Aidha Kamanda MISIME amesema wamekamatwa raia wawili kutoka
Ethiopia katika eneo la Nala Dodoma Mjini wakiwa hawana kibali cha
kuingia nchini na kuishi. Watu hao ni GETHGACHEW ANCHISO mwenye miaka
29, na KONJITI FEYSA mwenye miaka 23.
Vilevile huko katika kijiji cha Tubugwe juu kata ya
Chamkoloma Tarafa ya Mlali Wilayani Kongwa amekamatwa mtu mmoja
anayefahamika kwa jina la MWAJABU SALUM mwenye miaka 28, mkulima, mkazi
wa Tubugwe juu akiwa amelima bhangi ndani ya shamba lake la mahindi la
hekari mbili na nusu (2 ½).
Kamanda MISIME ametoa wito kwa wakulima kutolima mazao
haramu na badala yake walime mazao yenye tija kwa maendeleo halali kwani
hatima ya wahalifu wanaolima bhangi na kukutwa na silaha bila kibali ni
kuishia jela na kuzitesa familia zao kwa vitendo wanavyofanya vya
kihalifu. Aidha amewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi
la Polisi kuwafichua watu wanaomiliki silaha kinyume cha sheria, kulima
na kumiliki au kuuza dawa za kulevya na kujihusisha vitendo vingine vya
kihalifu katika maeneo yote ya Mkoa wa Dodoma kwa usalama wa wananchi
kwa ujumla na kutokomeza uhalifu wa aina zote.
Bhangi ikiteketezwa baada ya kukamatwa katika shamba la mahindi.
Watuhumiwa waliokuwa wakilima Bhangi hiyo.
Bhangi ikiteketezwa baada ya kukamatwa katika shamba la mahindi.
Watuhumiwa waliokuwa wakilima Bhangi hiyo.
Post a Comment
Click to see the code!
To insert emoticon you must added at least one space before the code.