0


Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chadema wamekosoa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kupata hati zenye mashaka na kueleza kuwa hesabu za vyama vyao zipo sahihi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Nape Nnauye na Mkurugenzi wa Fedha wa Chadema, Anthony Komu walidai taarifa ya CAG ndiyo yenye upungufu.
Nape katika mahojiano maalumu na waandishi wa habari yaliyorushwa moja kwa moja na kituo cha Radio 5 Arusha alisema, kuna tatizo la kutokubaliana kutokana na ukaguzi wa CAG.
Alisema mahesabu ya CCM yanayotokana na fedha za ruzuku kutoka serikalini yapo sahihi lakini wana mgogoro na CAG ambaye anataka mahesabu juu ya mali zote za CCM.“CCM ina miradi mingi kwa mfano hapa Arusha tuna uwanja wa Sheikh Amri Abeid awali uwanja huu, ulikuwa unasimamiwa na Mkoa wa Arusha pekee, sasa mkoa umegawanywa siyo rahisi kuwa na mahesabu yote,” alisema.
Alisema kwa maagizo ya CAG, kuandaa hesabu na taarifa za mali zote za CCM, inahitaji kutumika kwa zaidi ya Sh1 bilioni jambo ambalo ni gumu.
“Sisi tunadhani CAG anapaswa kukagua mahesabu ya fedha za ruzuku tunazopewa na Serikali lakini siyo mahesabu ya mali zote za CCM,” alisema.
Kwa mujibu wa taarifa ya CAG, ameainisha vigezo saba tofauti vilivyosababisha hesabu za CCM kupata hati yenye mashaka na kueleza kuwa CCM imekosa uhalali wa kisheria kumiliki baadhi ya mali ilizonazo.
Ukaguzi huo wa CAG umefanyika kwa mujibu wa Sheria namba 5 ya mwaka 1992 ya Vyama vya Siasa, iliyofanyiwa marekebisho na Sheria namba 7 ya mwaka 2009, inayompa CAG mamlaka ya kukagua hesabu za vyama vya siasa.
Ilibainisha vigezo vingine vya hati yenye mashaka kuwa ni CCM kutowasilisha taarifa ya mapato yake ya fedha kutoka kwa wafadhili mbalimbali zilizofikia Sh1,526,536,802, huku CAG pia akishindwa kupata nyaraka za kuthibitisha matumizi na malipo yaliyofanywa na chama hicho yanayofikia Sh6,045,438,052.
Kwa upande wa Chadema, Komu alisema ripoti ya CAG ina upungufu kwani, inataka chama hicho kuandaa taarifa za mahesabu na uthamini wa mali hadi mikoani.
“Mapungufu (upungufu) ambayo alianisha ya kutofanya uthamini wa mali zetu kutokuwa na mahesabu ya benki katika ngazi mbalimbali na vitabu vya risiti kwa baadhi ya maeneo ni mambo ambayo huwezi kuyakamilisha kutokana na mfumo wa vyama vyetu,” alisema.
Alikiri kuwa chama kuwa na akaunti nyingi kwa madai kuwa kila mkoa, wilaya na jimbo wana akauti yao.(Mwananchi)

Post a Comment

 
Top