0
 
Rais Jakaya Kikwete akiongozwa na Naibu Mkurugenzi wa kituo cha televisheni cha Azam TV, Tido Mhando (kushoto)na msimamizi wa vipindi, Yahya Mohamed wakati wa uzinduzi wa studio za televisheni hiyo jijini Dar es Salaam jana. Picha na Emmanuel Herman 
Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete amesema haoni tatizo kwa vyombo vya habari kuandika kashfa zinazoibua mijadala kwenye jamii kwa kuwa yanasaidia uongozi kujirekebisha, lakini akaonya kuwa vyombo hivyo  vikitumia uhuru wao kuchochea chuki, vurugu na mifarakano, Serikali haitavumilia.
Rais Kikwete alikuwa akijibu swali kutoka kwa Tido Mhando wa Azam Media kuwa, anajisikiaje pale vyombo vya habari vinapoibua kashfa nzito kama za uchotwaji fedha kwenye akaunti ya escrow na mkataba wa uzalishaji umeme wa Richmond ambazo alisema zilionekana kutikisa Serikali.
Tido alimuuliza swali hilo wakati wa mahojiano maalumu kwenye hafla ya uzinduzi wa studio za kituo cha televisheni cha Azam TV jana.
“Sioni tatizo,” alisema Rais Kikwete kwenye mahojiano hayo.
Alisema hachukizwi na habari hizo na hana tatizo na vyombo vya habari, kwani kwa namna moja au nyingine zinasaidia Serikali yake kujiimarisha na kufanya kazi kwa weledi zaidi.
“Ukiandika masuala ya uchochezi, lazima tutakuchukulia hatua, lakini mkiandika kuikosoa CCM, hilo sina shida nalo,” alisema Rais Kikwete.
Licha ya kauli hiyo, Rais Kikwete alisisitiza  kuwa, “Tunatakiwa tuwe na uhuru unaozingatia weledi katika utendaji wa kazi …Serikali haiwezi kuvumilia kuona baadhi ya vyombo vya habari vinatumia uhuru huo kuchochea chuki, vurugu na mifarakano katika nchi.”
Akiwa katika moja ya studio zilizoanza kurusha taarifa ya habari ya saa mbili usiku jana, aliendelea kueleza kuwa, machafuko yaliyowahi kutokea Rwanda yalichochewa na vyombo vya habari hadi kufikia hatua wananchi wengine wakawa wanaitwa mende.
Uzinduzi ambao ulifuatiwa na uzinduzi wa jiwe la msingi pamoja na gari la kurusha matangazo moja kwa moja, (Outside Broadcasting -OB van).
Ilipofuatiwa hotuba yake, Rais Kikwete alitumia wasaa huo kummwagia sifa, mmiliki na Mwenyekiti wa Kampuni za Azam, Said Salim Bakhresa kwa uwekezaji wa studio hizo za kisasa.
“Uwekezaji uliofanywa kwa studio hizi za kisasa ni mkubwa. Hakuna uwekezaji kama huu uliowahi kufanywa katika sekta ya habari na utangazaji nampongeza sana Said Bakhressa kwa uwekezaji huu,” alisema Rais Kikwete na kuongeza kuwa, studio hizo zinaongoza kwa ukubwa Afrika Mashariki na Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Alisema, uzinduzi wa studio hizo zilizogharimu Dola 31 milioni za Marekani sawa na Sh55 bilioni za Tanzania, utapanua wigo wa ajira, utafungua ukurasa mpya katika tasnia hiyo na kwamba italeta chachu ya ushindani kwa vyombo vya habari vingine nchini na Afrika.
“Tunaamini studio hizi zitatoa huduma bora zenye kuzingatia maadili kama mlivyosema kuwa ubora ndiyo msingi wenu, bila kusahau kuwaendeleza waandishi wenu kwa mafunzo na  na kujali maslahi yao ili wafanye kazi vizuri.
“Bila kufanya hivyo weledi na uadilifu katika kazi utashuka,” alisema na kuongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikana na chombo hicho.
Aliongeza kuwa, uandaaji wa vipindi na maudhui yao yazingatie utaifa. “Msije kujifanya wa kimataifa na kusahau utaifa, hata CNN ni Marekani kwanza, Al-Jazeera ni Qatar kwanza na BBC ni Uingereza kwanza na dunia baadaye,” alisema.
Kwa upande wake, mwenyekiti huyo aliishukuru Serikali kwa kutoa fursa kwa watu binafsi kuwekeza katika sekta ya utangazaji na habari.
“Tutaendelea kuwahudumia Watanzania kwa kusambazia taarifa muhimu na bora kwani ubora ndiyo silaha yetu,” alisema Bakhressa, ambaye ni mmiliki wa Azam Media.
Waalikwa zaidi ya 200 walishuhudia uzinduzi wa studio hizo ambazo Rais alisema kuwa zitaleta ushindani miongoni mwa vituo vya televisheni.
CHANZO:MWANANCHI

Post a Comment

 
Top