Mwenyekiti wa CUF, Prof Ibrahim Lipumba, akisikiliza maelezo ya Matern
Kayera wa kitengo cha habari za papo kwa papo cha Mwananchi
Communications Ltd (MCL) alipotembelea ofisi hizo Dar es Salaam jana.
Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Francis Nanai na Mhariri Mtendaji
Mkuu, Bakari Machumu.
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa
Ibrahim Lipumba amesema hana mpango wa kugombea ubunge katika Uchaguzi
Mkuu wa Oktoba mwaka huu kama ambavyo imekuwa ikidaiwa.
Vilevile Profesa Lipumba ambaye pia ni mwenyekiti
mwenza wa Ukawa, hakukubali wala kukataa alipoulizwa iwapo atajitosa
kuomba ridhaa ya kupeperusha bendera ya umoja kwa nafasi ya urais.
“Mimi naulizwa na ninasikia wanasema nitagombea
Temeke au Tabora Kaskazini. Mimi sina utaratibu wala sijaota na sina
mpango wowote wa kugombea ubunge,” alisema alipotembelea ofisi za gazeti
hili, Tabata Relini Dar es Salaam jana.
Profesa Lipumba akijibu swali kama hakuwa na
mpango wa kugombea ubunge, je, ana mpango wa kugombea urais kupitia
Ukawa, alijibu; “Sasa nani atakuwa mgombea hilo ni jambo ambalo (Ukawa)
hatujalifanyia uamuzi, bado lipo katika utaratibu,” alisema na kuongeza;
“Siwezi kusema kwamba nitagombea nafasi ya urais
kwa sasa, mgombea ndani ya umoja wetu bado hajapatikana kama atatoka nje
ya CUF mimi nitamuunga mkono atakayependekezwa.”
Tangu Novemba mwaka jana vyama vya CUF, Chadema,
NCCR-Mageuzi na NLD vimekuwa katika majadiliano ya kuachiana nafasi
katika majimbo ya uchaguzi kwa nafasi za ubunge na udiwani ili viweze
kusimamisha mgombea mmoja kila sehemu lengo ni kuishinda CCM.
Lipumba amegombea urais mara nne, akiwa ameshika
nafasi ya pili mwaka 2000 na 2005 na mwaka 2010 kushuka hadi nafasi ya
tatu nyuma ya Dk Slaa na Rais Jakaya Kikwete.
Profesa Lipumba akizungumzia suala Mbunge wa
Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe na iwapo kuna mazungumza ya kujiunga CUF,
alisema suala hilo ni nyeti hasa ukizingatia na mazingira yake yaliyopo
ya sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow.
“Sijapata fursa ya kuzungumza naye (Zitto) lakini
sina taarifa yeyote kama anakuja CUF au nini kwani uanachama ni suala
linalofanyika ngazi ya tawi siyo huku Taifa.”
“Zitto ana akili sana, anajua kuchambua na kujenga
hoja lakini naheshimu kwa wenzetu wa Chadema kwa muda mrefu wamekuwa na
hoja nzito kuhusu yeye. Kwa kuwa hawa tuna ushirikiano, basi hatuna
budi kukubaliana nao.
Post a Comment