Ofisi za jengo la tawi la Chama cha Wananchi (CUF)
Jimbo la Dimani, mkoa wa Mjini Magharibi, limeteketea kwa moto na
kusababisha hasara kubwa ya vitu vilivyokuwamo humo ingawa thamani ya
vitu hivyo haijajulikana.
Tukio hilo lilitokea mtaa wa Kisauni usiku wa kuamkia jana saa nane usiku.
Mashuhuda walisema watu wasiojulikana walifika na gari aina ya
Pick-up na kuvunja mlango wa ofisi hizo na kulilipua jengo hilo kwa
petroli.
“Majira ya saa nane usiku ilikuja gari na watu wawili walishuka
katika gari hiyo na kuingia ndani huku wakisikika wakisema tayari
tuondoke na baada ya kuondoka tu jengo hilo lililipuka,” alisema shuhuda
mmoja aliyekuwapo katika eneo hilo.
Alisema baada ya kuona moto na moshi mkubwa ukiwa umetanda ndipo walipowapigia watu wa Zima Moto na walifika kuuzima.
Diwani wa wadi ya Tomondo, Hassan Hussen Yussuf, alisema hali
inasikitisha katika harakati za kisiasa kuona Zanzibar inarejea katika
siasa za chuki na uhasama.
“Matukio kama haya hutokea karibu na uchaguzi kwa kweli
inasikitisha sana na kama halii itaendelea itakuwa hatari katika nchi,”
alisema Yussuf.
Alisema katika jengo hilo kulikuwa na vifaa mbalimbali vya thamani
na fedha taslimu za malipo ya uchukuaji wa fomu za wagombea
walizolipia zimeteketea.
Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salum
Bimani, alisema CUF kinalihusisha tukio hilo kuwa ni joto la uchaguzi
na kuwashutumu waliofanya waliofanya tukio hilo kwani matukio kama hayo
yamekuwa yakifanywa inapokaribia kipindi cha uchaguzi mkuu.
“Hujuma hizi zimepangwa na ni za makusudi kuchafua amani ya nchi,na
hali kama hii hutokea zaidi karibu na uchaguzi na CUF hufanyiwa
hujuma mbalimbali ikiwamo kuchomwa moto ofisi zetu,” alisema Bimani.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam,
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa Jeshi la Polisi
linaendelea na uchunguzi.
SOMA ZAIDI HAPA
Post a Comment