RAIS JAKAYA KIKWETE
Vuguvugu la kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba limeshika kasi hivi sasa.
Tumeshuhudia baadhi ya wanasiasa wakitangaza nia
na tumejionea makundi kadhaa katika jamii yakijitokeza ‘kuwaomba’ wale
yanaowaona kuwa na sifa kujitokeza kuomba kupitishwa na vyama vyao
kuwania nafasi hiyo ya juu kabisa katika uongozi wa nchi. Kwa vyovyote
vile, uchaguzi wa mwaka huu utakuwa na hamasa, msisimko na kila aina ya
mbinu kulinganisha na uliopita hasa ikizingatiwa kwamba safari hii Taifa
litalazimika kumpata Rais wa Awamu ya Tano.
Hiyo ina maana kwamba ndani ya chama tawala, joto
la kumpata mgombea urais halitakuwa kama ilivyokuwa miaka mitano
iliyopita kwani hata waliokuwa na nia au tamaa ya nafasi hiyo, walijua
fika kwamba wasingeweza kubadili utaratibu wa chama chao kwani Rais
Jakaya Kikwete alikuwa amemaliza kipindi kimoja tu kati ya viwili
anavyoruhusiwa kwa mujibu wa sheria za nchi.
Safari hii, Rais Kikwete anang’atuka, tumeshuhudia na kusikia kila aina na patashika za wanaCCM wanaowania kumrithi.
Lakini uchaguzi wa safari hii, tofauti na mwingine
wowote uliowahi kufanyika chini ya mfumo wa vyama vingi tangu mwaka
1995, tutashuhudia upinzani ulio imara na uliojipanga vizuri zaidi.
Tofauti na miaka iliyopita, vyama vikubwa vya
upinzani chini ya mwamvuli wao wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),
vimeamua na vimeanza mchakato wa kupata jina moja tu la mgombea urais.
Hiyo ikimaanisha kwamba kutakuwa pia na vuguvugu kubwa la wanasiasa
kuwania kupitishwa na umoja huo.
Kutokana na sababu hizo tulizozitaja. Tunaamini
kwamba hali ya kisiasa katika taifa hasa katika kipindi hiki cha kusaka
wagombea siyo katika urais tu, bali ubunge na udiwani itakuwa ngumu na
ya wasiwasi mkubwa.
Tayari tumeshaanza kusikia vilio vya rafu kutoka
kwa wanasiasa wenyewe kwa wenyewe na hata wananchi, mambo ambayo
tunaamini kwamba yasipofanyiwa kazi kwa maana ya kuyadhibiti, hali
inaweza kuwa mbaya.
Kwanza, vyama husika vinapaswa kufungua milango na
kuruhusu wanachama wake kujitangaza na siyo kutoa ruhusa inayoambatana
na masharti na vigezo vigumu.
Tunaamini kwamba hiyo ndiyo njia sahihi ya kumpata
rais mwenye vigezo hasa ikizingatiwa kwamba hakuna sifa za kitaifa za
kumpata rais wa nchi, ukiondoa zile za vyama hivyo, ruhusa hiyo ingetoa
mwanya kwa vigezo vya maadili ya kijamii na utamaduni kutumika
kuwachuja.
Lakini pia tunadhani kwamba hiki ni kipindi muhimu
cha elimu ya uraia, wananchi wanatakiwa kujengewa uwezo wa kuelewa
maana ya ushindani wa kisiasa ambao hautaliingiza Taifa katika
machafuko.
Hiki ndicho kipindi cha kuanza kuwajenga wananchi
kifikra kuelewa mchakato mzima wa uchaguzi na siyo kusubiri dakika za
lala salama.
Lakini pia hiki ndicho kipindi cha kuwajenga wananchi
kisaikolojia, kumpokea kiongozi mpya wa nchi ambaye atakuwa na dhamana
ya kuliongoza Taifa hili, pengine kwa muongo mwingine mmoja.
Tunapenda kusikia kauli kutoka Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC), vyama vya siasa na wadau wengine juu ya masuala haya
muhimu kwa mustakabali wa taifa hili kwa miaka mingine mitano.
Tunachelea kusema kwamba haya yasipofanyiwa kazi kwa makini, patashika
hii ya kupata viongozi ikianza tunaweza kujuta.MWANANCHI
Post a Comment