Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete amelikata
Jeshi la Polisi nchini kujiandaa kikamilifu ili kukabiliana na vurugu
zozote zitakazojitokeza wakati wa uandikishaji wapigakura, upigaji Kura
ya Maoni ya kupitisha Katiba Inayopendekezwa na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba,
mwaka huu.
Akifunga mafunzo ya maofisa warakibu wasaidizi
katika Chuo cha Taaluma ya Polisi, Dar es Salaam jana, Rais Kikwete
alisema dalili zinaonyesha kwamba kuna watu wenye nia ya kuhatarisha
amani katika matukio hayo.
“Tunayoyasikia na tunayoyaona yanaashiria kuwapo
kwa dalili za wenzetu kukwamisha shughuli hizi za kitaifa kwa kufanya
vurugu, Jeshi la Polisi jiandaeni na vitendo vyote vitakavyofanywa kwa
lengo la kuhatarisha amani,” alisema akijibu maombi ya kupatiwa vifaa
yaliyowasilishwa kwake na Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu.
Alisema Serikali itahakikisha kazi ya uandikishaji
katika daftari la wapigakura, upigaji wa kura ya maoni na uchaguzi mkuu
vinafanyika kwa amani na utulivu kwa gharama zozote.
Alisema ili kufanikisha kazi hiyo, Serikali
italiwezesha Jeshi la Polisi ili litekeleze kikamilifu majukumu yake ya
kulinda amani na utulivu.
“Tutawawezesha kwa kuwapa vifaa ili kuhakikisha
mnafanya kazi yenu ya kutunza amani kwa umakini zaidi,” alisema Rais
Kikwete anayemaliza muda wake wa mihula miwili ya urais baada ya
uchaguzi mwaka huu.
Iwapo mambo yote yatakwenda kama yalivyopangwa,
Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa itapigwa Aprili 30 wakati
Uchaguzi Mkuu utafanyika Oktoba.
Profesa Lipumba apinga
Akizungumzia kauli hiyo ya Rais Kikwete,
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema, “Rais Kikwete yeye
ndiye mtu wa kwanza kuivuruga amani kwa kutangaza tarehe ya kufanyika
kwa kura ya maoni wakati siyo jukumu lake na jukumu hilo ni la NEC,
Serikali yake kushindwa kuratibu vyema mchakato wa uandikishaji.
“Kama uandikishaji hauendi vizuri mpaka sasa,
anavunja sheria za nchi halafu yeye mwenyewe tena anakwenda kwa vyombo
vya dola na kuvieleza vijiandae wakati yeye huyohuyo ndiye ameanzisha
uvunjifu wa amani tunashindwa tumweleweje,” alisema.
Profesa Lipumba alisema kinachotakiwa kufanyika
kwa sasa ni NEC kutangaza tarehe kamili ya uchaguzi na uandikishaji
uende kwa utaratibu tofauti na ilivyo sasa kwa mkoa mmoja wa Njombe
kusuasua mambo ambayo yanaashiria uvunjifu wa amani.
Kuhusu rushwa
Akizungumzia tuhuma za rushwa dhidi ya polisi, Rais Kikwete
alisema tafiti mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanyika nchini zinaonyesha
kwamba taasisi hiyo bado inaongoza kwa rushwa.
“Bado kuna wenzenu wachache ambao wanachukua
rushwa, wachukulieni hatua ili mwondokane na aibu hii, msikubali watu
wachache waharibu sifa nzuri ya Jeshi la Polisi,” aliagiza.
Roho mbaya
Kikwete aliutaka uongozi wa Jeshi la Polisi
kujenga utamaduni wa kuwapandisha vyeo askari polisi ili kuwaongezea ari
ya kufanya kazi.
“Zamani viongozi wa polisi walikuwa na roho mbaya
hawakuwa wakiwapandisha vyeo askari, nikawauliza kwa nini, lakini
hawakuwa na majibu, inasikitisha vyeo vipo lakini mtu anasota kwa miaka
mingi na kacheo kale kale, acheni roho mbaya pandisheni vyeo askari kila
inapobidi,” alisema.
Alisema kuna umuhimu wa kuwa na jeshi lenye wasomi wengi ili waweze kukabiliana na mbinu mpya za uhalifu.
“Wahalifu wanaendelea kubuni mbinu za kila aina, tunatakiwa kuwa na wasomi ambao wataweza kukabiliana na mbinu hizo,” alisema.
Aliutaka uongozi wa jeshi hilo kuongeza idadi ya
polisi wanawake ili kuimarisha dawati za jinsia kwenye vituo vya polisi,
kitendo kitakachopunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Ujambazi
Kuhusu ujambazi, Rais Kikwete alisema katika kipindi chake, jeshi hilo limefanya kazi kubwa katika kukabiliana na ujambazi.
“Wakati naingia madarakani nilikuta matukio ya
majambazi kuingia na kuiba fedha hadi benki, matukio hayo yalikuwa ya
kawaida kuyasikia, nikasema majambazi hayawezi kuachwa yatambe,”
alisema.
Alisema hivi sasa matukio hayo yamepungua kwa
kiasi kikubwa na akalipongeza jeshi hilo kwa kazi nzuri ingawa bado kuna
matukio machache.
Awali, IGP Mangu alimwomba Rais Kikwete kuliwezesha jeshi hilo
kivifaa ili liweze kujiandaa mapema na upigaji wa kura ya maoni na
uchaguzi mkuu.
“Tunaomba tuwezeshwe vifaa mapema ili tuweze
kuvifanyia mazoezi kabla ya upigaji wa kura ya maoni na uchaguzi mkuu wa
rais, wabunge na madiwani baadaye mwaka huu,” alisema.
Mkuu wa Chuo cha Maofisa wa Polisi Dar es Salaam,
Ali Lugendo alisema askari 290 wamehitimu mafunzo hayo na hivi sasa
watakuwa warakibu wasaidizi wa polisi.
Alisema wahitimu hao watakwenda kuwa viongozi
kwenye vituo mbalimbali vya polisi vya wilaya na hivyo kuwa wasimamizi
wa nidhamu kwa askari.MWANANCHI
Post a Comment