0
Katibu wa TFF, Selestine Mwesigwa.
Na Nicodemus Jonas,Dar es Salaam
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limesema timu zenye rekodi mbaya ya kuachana na wachezaji kwa migogoro, zipo hatarini kufungiwa kuendelea kusajili.Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa TFF, Selestine Mwesigwa, kufuatia vitendo vya wachezaji au waajiriwa wengine wa timu kuzua malalamiko mara kadhaa ya kutolipwa stahiki zao baada ya kuachana.
Simba na Yanga ndiyo vinara wa rekodi hiyo mbaya huku kesi iliyopo sasa ikiwa ni ya straika wa Yanga, Amissi Tambwe, anayeidai Simba zaidi ya Sh milioni  11 kufuatia kukatisha mkataba wake katikati ya msimu huu.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Mwesigwa alisema klabu kariba ya Simba zisipobadilika, zitajikuta matatani kwa kufungiwa.
“Sisi kama shirikisho tupo kwa ajili ya maslahi ya mpira wa miguu, haipendezi kuona kila siku mnapokea malalamiko ya namna hii (akizungumzia sakata la Tambwe) na itafika hatua tutazisimamisha kusajili.
“Kama yakiendelea, tutazionya iwe kwa maandishi au kauli, lakini kinyume cha hapo ni kuzifungia usajili ili iwe fundisho,” alisema katibu huyo wa zamani wa Yanga.
Msimu uliopita, Yanga ilizuiwa mapato ya mlangoni kwa agizo la mahakama kwa ajili ya kuwalipa wachezaji wake wa zamani, Steven Marashi na Wisdom Ndlovu waliositishiwa mkataba.

Post a Comment

 
Top