Na Mwandishi Maalum, New York
Mkuu wa
Majeshi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jenerali Davis Mwamunyange,
amelishauri Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, kuweka
bayana na kwa uwazi mamlaka ( mandate) ambayo misheni ya kulinda
Amani itapaswa kutelekeza kule inakopangiwa kwenda.
Ametoa
ushauri huu siku ya Alhamisi wakati alipokuwa akitoa mchango wake
kwenye mkutano wa Wakuu wa Majeshi ya Ulinzi ambao nchi zao zinachangia
katika operesheni za ulinzi wa Amani za Umoja wa Mataifa.
Katika
mkutano huo uliokuwa wa siku moja, na kuhudhuriwa na Wakuu wa Majeshi
na Maafisa wa Ngazi za Juu ,kutoka nchi 108, Jenerali Mwamunyage
amesema;
“ Wakati
wa utoaji wa idhini na mamlaka kwa misheni ya kulinda Amani, Baraza
Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, linatakiwa kumwita mbwa kwa jina
lake kama lilivyo.Mbwa aitwe kwa jina lake. Elezeni bayana na kwa
uwazi mamlaka na idhini za utekelezaji za ya misheni ”
Na
kuongeza, “ iwekwe wazi, kama ni misheni ya kulinda Amani, basi ielezwe
ni ya kulinda Amani, na kama ni ya matumizi ya nguvu basi na iwe
hivyo”. Amesisitiza Mkuu wa Majeshi
Amesema
kwamba, kwa kutamka jina halisi /mamlaka ya misheni pale inapoundwa,
Baraza Kuu la Usalama linakuwa linapeleka ujumbe ulio sahihi kwa pande
zote zinazohusika pamoja na nini wakitarajie.
Jenerali
Mwamunyage ameuleza washiriki wa mkutano huo mkutano wa kwanza wa aina
yake kuwakutanisha Wakuu wa Majeshi zaidi ya mia moja, wakati mmoja na
mahali pamoja. Kwamba, uwazi huo pia utasaidia kuweka bayana hatua za
utekelezaji zinazofanywa na walinzi wa amani kwenye eneo la
utekelezaji.
Vile vile
Mkuu wa Majeshi ya Tanzania ameshauri pia kuwa misheni ambayo tangu
kuundwa kwake zilikuwa na mamlaka ya kutumia nguvu, ni vema
zisiendelee kutambuliwa hivyo pale mamlaka ya misheni hiyo
yanapobadilika kutoka matumizi ya nguvu na kuwa misheni ya kulinda
Amani au jina lolote lile.
Tanzania
inawanajeshi wake katika Misheni mbalimbali ikiwa ni pamoja na
UNAMID ( Darfur) UNFIL, ( Lebanon) MONUSCO ( DRC) na katika maeneo
mengine. Vile vile Tanzania ina Polisi na Askari Magereza ambao nao
wanahudumu katika misheni mbalimbali.
Akizungumzia
kuhusu mkutano huo ambao ulifunguliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa na Ban Ki Moon na kufungwa na Naibu Katibu Mkuu Jan Eliasson.
Jenerali Davis Mwamunyange amesema, mkutano kama huo unapashwa
kuitishwa mara kwa mara kwa kuwa unawawezesha wakuu wa majeshi
kubadilishana uzoefu wao katika utekelezaji wa operesheni za ulinzi wa
Amani na hasa kwa kuzingatia kwamba nchi wanachama ndio wanaotoa
wanajeshi wao na ndio haswa wanaokumbana na changamoto mbalimbmali za
utekelezaji wa dhamana hiyo.
Awali
akifungua mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon
pamoja na kuwashukuru Wakuu hao wa Majeshi kwa mchango wao katika eneo
hilo la ulinzi wa Amani, amesema operesheni ya kulinda Amani chini
ya Umoja wa Mataifa, licha kwa kwamba ni dhamana inayohitajika sana
lakini pia inakabiliwa na changamoto mbalimbali.
Akazitaja
baadhi ya changamoto hizo kuwa ni upugufu wa raslimali fedha, zana,
vifaa na teknolojia za kisasa lakini pia ugumu na hatari wanazokumbana
nazo walinzi wa Amani, ambapo hivi sasa mbinu za kigaidi na uvamizi kwa
walinzi wa Amani ni baadhi ya changamoto na hatari wanazokumbana nazo.
Katibu
Mkuu, amewataka wakuu hao wa majeshi kuongeza ushirikiano wao kwa Umoja
wa Mataifa na hasa katika kutafuta mbinu za kukabiliana na changamoto
za kiulinzi na kiusalama ambazo duni hivi sasa inakabiliana nao.
Akaongeza
kuwa kujitokeza kwa idadi kubwa ya wakuu hao wa majeshi ya ulinzi
kushiriki mkutano huo, kumeipa faraja kubwa Umoja wa Mataifa.
Naye
Naibu Katibu Mkuu Jan Eliasson, akihitimisha mkutano huo, amewataka
wakuu hao wa majeshi na serikali zao kuendelea na majadiliano ya
mchakaTo wa kuundwa kwa majeshi ya ulinzi ya kikanda, majadiliano
ambayo yanatakiwa kuendelea kuelekea mkutano wa Operesheni ya Ulinzi
wa Amani utakaofanyika mwezi Septemba mwaka huu.
Wakuu hao
wa Majeshi ya Ulinzi pamoja na kutoa mchango wa mawazo yao, pia
walipata fursa ya kupata maelezo kutoka kwa Viongozi wakuu waandamizi
wanaoongoza Idara zinazozohusu Operesheni ya Ulinzi wa Amani.
-------------------------------------------------------
HABARI KATIKA PICHA
" Mnatuwakilisha vema?" ndilo swali ambalo Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi,
Jenerali Mwamunyange alilowauliza watanzania hawa wawili, Afisa wa
Usalama wa UN Bw. Jacob Mwashiozya na Bw. Joseph Msami, wa Idhaa ya
Kiswahili ya Umoja wa Mataifa walipokuwa wakisalimiana naye na ujumbe
wake mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa wakuu wa majeshi ya ulinzi
Jenerali Davis Mwamunyange (watatu kushoto), akiwa na ujumbe wake mbele
ya bendera ya Tanzania, baada ya kumalizika kwa mkutano wa siku moja wa
Wakuu wa Majeshi ya Ulinzi kutoka nchi 108. Kutoka kushoto ni Kanali
Adolf Mutta, Brigedia Jenerali Luwogo, Brigedia Jenerali Kamunde, Meja
Ngh'abi, na Luten Kanal Itang'are
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, akiingia kwa staii ya
aina yake wakati alipokwenda kufungua mkutano wa kwanza wa aina yake
kufanyika katika Umoja wa Mataifa, ambapo Wakuu wa Majeshi ya ulinzi
kutoka nchi zaidi ya 100 walikutana kwa wakati mmoja na mahali pamoja
kujadiliana na kubadilishana mawazo kuhusu operesheni za ulinzi wa amani
za umoja wa mataifa.
Post a Comment