Rahma
Mashamu ambaye ni mama mzazi wa watoto wawili mmoja wa miaka 11 na
mwingine 15 wanaodaiwa kubakwa na baba wa watoto hao akilia kwa uchungu
wakati akihojiwa na waandishi wa habari kuhusiana na tukio hilo,
wilayani Kibaha mkoani Pwani.
Mkazi mmoja
wa Miembe Saba wilayani Kibaha mkoani Pwani amekamatwa na polisi
akituhumiwa kuwabaka watoto wake wawili wadogo kwa zaidi ya miaka miwili
sasa.
Habari
zilizolifikia gazeti hili, zilisema kuwa katika tukio hilo ambalo
limethibitishwa na polisi na watoto wenyewe, baba huyo alianza
kuwafanyia binti zake vitendo hivyo mwaka 2013 kwa siku ambazo mkewe
ambaye nimama wa wasichana hao hakuwapo hadi usiku wa Machi 19, mwaka
huu. Kwa sasa tunayahifadhi majina ya familia hiyo.
Watoto hao
mmoja mwenye umri wa miaka 15 anayesoma darasa la saba na mdogo wake
mwenye umri wa miaka 11 aliyeanza kubakwa akiwa darasa la tatu.
Kwa mujibu
wa watoto hao, baba huyo alikuwa anamuita mmoja wa watoto wake chumbani
kwake na kumtaka alale na mdogo wao wa kiume wakati huo akiwa na mwaka
mmoja na binti akipitiwa na usingizi humvua nguo za ndani na kumwingilia
huku akimtaka kukaa kimya na kuvumilia maumivu.
Mke wa
mtuhumiwa huyo, ambaye amekuwa akizimia mara kwa mara kutokana na kulia
baada ya kubaini mchezo huo, alisema aligundua watoto wake wanabakwa
Ijumaa iliyopita baada ya mmoja wa mabinti zake hao kumweleza kuwa baba
yake alikuwa amembaka Machi 19, mwaka huu.
Alisema
kabla ya binti huyo kumweleza hivyo, alimwomba asimpige kwani kuna kitu
anataka amweleze, japo ni kibaya lakini yeye amechoshwa na kimekuwa
kikimuumiza kichwa.
“Alisema
kila ninapokwenda katika biashara zangu, anatamani nisiwe ninawaacha
hapo, nikamwahidi sitamfanya kitu ili mradi aseme ukweli tu,” alisema
mama huyo.
Baada ya
kuhakikishiwa kulindwa, ndipo binti huyo aliposimulia jinsi ambavyo baba
yake amekuwa akiwafanyia na kuwatishia wakipiga kelele atawaua.
“Niliposikia
mwili ulisisimka na ghafla binti yangu mwingine naye akatokea akilia na
kuniambia, ‘hata mimi baba ananifanyiaga hivyohivyo kila siku unapokuwa
umepeleka mboga sokoni Kariakoo,” alisema mama huyo.
Mwanamke
huyo ameomba sheria ichukue nafasi yake katika tukio hilo kwa kuwa ni la
kinyama na pia wataalamu wa saikolojia wamsaidie binti yake mdogo wa
darasa la tano kwani yeye ameathirika zaidi.
Daktari aliyewapima watoto hao, ameshauri binti huyo mdogo apate ushauri zaidi ili kurudisha akili yake katika hali ya kawaida.
Simulizi za watoto
Wakizungumza
nyumbani kwao jana watoto hao, walisema baba yao alikuwa akiwatishia
kuwakatakata kwa panga au kuwakaba koo humohumo chumbani endapo
wangethubutu kumweleza mtu yeyote kitendo wanachokifanya.
“Tulikuwa
tumeingia kwetu kulala na wadogo zangu, nikasikia ananiita
nikambembeleze mtoto eti anamsumbua, nilikwenda nikambembeleza akalala,
wakati nashuka kitandani kurudi chumbani kwetu baba akanivuta kwake
akanivua, akasema anachokifanya ni suna kwa hiyo hataki kelele, akisikia
atanikaba nife.”
“Niliumia
sana na asubuhi mama alirudi nikajitahidi kweli asijue na hata shule
sikwenda, jioni mama aliondoka tena baba hakuniita siku hiyo lakini
baada ya siku tatu aliniita tena ikawa vilevile navumilia. Siku
zilivyozidi unaweza kukuta kwa wiki naitwa hata mara nne siku ambazo
mama hayupo nyumbani,” alisema.
Watoto hao
walieleza kuwa baadaye baba huyo alihamia kwa binti mdogo kwa staili
ileile na kila mmoja alikuwa akiitwa kwa zamu na kwa vile kila mmoja
alijua ni siri yake na baba. Kutonaka na woga wa kuuawa, hakuna
aliyemweleza mwenzake hadi katikati ya mwaka jana mmoja wao alipomweleza
mwenzake na baadaye kumweleza mama yao.
“Baba
alikuwa anasema atatuua bila hata mtu kujua na tutaozea shambani, hata
nikiwa katika siku zangu baba ananiingilia hivyohivyo, naugua kila mara
UTI, mdogo wangu naye kila mara UTI, tukaamua liwalo na liwe kama kufa
basi ila mama ajue,” alisema mtoto huyo huku akibubujikwa na machozi.
Mwenyekiti
wa Serikali ya Mtaa wa Miembe Saba, Hamis Shomari alisema kabla ya
kupelekwa kituo cha polisi Kongowe Jumamosi iliyopita, watoto hao
waliitwa shuleni hapo na kuhojiwa kila mmoja peke yake na wote walikiri
kuanza kubakwa mwaka 2013 na baba yao na kwamba tabia hiyo iliendelea
hadi Machi 19 usiku alipobakwa binti mdogo kwa mara ya mwisho na Machi
20 walipoamua kumweleza mama yao.
Kamanda wa
Polisi mkoani Pwani, Ulrich Matei alisema wanamshikilia mtuhumiwa huyo
na kwamba wasichana hao wamefanyiwa vipimo mbalimbali na majibu ya
daktari yamethibitisha kuwa wamebakwa na sehemu zao za siri
zimeharibiwa, hivyo wanaendelea na matibabu.
Habari na Picha na Julieth Ngarabali
Post a Comment