Naibu kamishna wa jeshi la polisi Mkoani Simiyu Charles Mkumbo
akiwaonyesha waandishi wa habari (hawapo pichani) baadhi ya sare za JWTZ
ambazo zilikamatwa askari wa jeshi la polisi Mkoani Simiyu pamoja na
Askari Magereza wilayani Bariadi
Baadhi ya noti bandia walizokutwa nazo
Naibu kamishna wa jeshi la polisi Mkoani Simiyu Charles Mkumbo
akiwaonyesha waandishi wa habari (hawapo pichani) baadhi ya pesa bandia
ambazo zilikamatwa askari wa jeshi la polisi
Sare zilizokamatwa.
Jeshi la polisi mkoani Simiyu linawashikilia askari wawili wa jeshi
la magereza na polisi kwa kukutwa na noti bandia ikiwa ni pamoja na sare
za jeshi la wananchi Tanzania (JWTZ).
Akitoa taarifa za kukamatwa kwa askari hao Naibu Kamishna wa jeshi la
polisi Mkoani Simiyu Charles Mkumbo alisema kuwa askari hao walikamatwa
juzi majira ya saa 9 mchana katika mtaa wa Old Maswa kata ya Nyakabindi
Wilayani Bariadi.
Alisema askari hao walifika kwenye kibanda cha M-pesa kinachomilikiwa
na Mwalimu wa Shule ya sekondari Old Maswa Kassian Luhende (29), wakiwa
na pikipiki yenye namba za usajili T-403 CXW aina ya Sunlg kwa lengo la
kuweka fedha hizo kweye simu.
Alisema baada ya Mwalimu huyo kupokea fedha kiasi cha noti 10 zenye
thamani ya Shilingi 10,000 alizitilia shaka ambapo alipoendelea
kuzikagua zaidi alizigundua kuwa siyo fedha halali.
Mkumbo alieleza kuwa Mwalimu huyo baada ya kugundua fedha hizo kuwa
ni feki, alichukua jukumu la kuwajulisha majirani zake ili kuomba Msaada
wa kuweza kuwakamata askari hao baada ya kugundua siyo watu wema.
Aidha alieleza kuwa baada ya mwalimu kutoa taarifa kwa majirani,
wananchi walikusanyika na kuanza kuwahoji askari hao, ndipo askari mmoja
alipotoa kitambulisho kuwa yeye ni askari na mwingine kujitambulisha
kuwa ni dereva bodaboda.
Alibainsiha kuwa wananchi baada ya kuambiwa hivyo waliwatilia shaka
zaidi ambapo walitoa taarifa Kituo cha polisi Bariadi, na askari kwenda
kuwakamata.
Mkumbo aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni askari mwenye namba H 2420 PC
Seleman Juma (25) ambaye ni askari wa kikosi cha kutuliza gasia FFU
Mkoani Simiyu, na askari namba B.6499 WDR Edmund Masaga (28) ambaye ni
askari Magereza wilayani Bariadi.
Kamanda Mkubo alieleza kuwa baada ya askari hao kukamatwa mmoja wao
PC Selemani Juma alipopekuliwa katika mfuko wa suruali yake alikutwa na
noti zingine za Bandia za elfu kumi kumi na jumla yake kama zingelikuwa
halali zingelikuwa na thamani ya Shilingi 1,920,000.
Mbali na hilo Mkumbo alieleza kuwa Askari huyo alipokwenda kupekuliwa
nyumbani kwake alikutwa na sare za JWTZ ambazo ni Pensi 4, T-shirt 2,
Kombati 1 pamoja na Kitambaa.
Hata hivyo Mkuu huyo wa polisi alieleza kuwa uchunguzi zaidi
unaendelea ili kubaini mtandao mzima wa usambazaji wa noti bandia ndani
ya mkoa huo, huku akieleza kuwa mara baada ya uchunguzi kukamilika
askari hao watachuliwa hatua za kinidhamu pamoja na kisheria.
Alitoa onyo kwa askari Mkoani Simiyu kuacha tamaa ya pesa na badala
yake waridhike na ajira zao zinazowapatia pesa halali, huku akieleza
kuwa kwa atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kisheraia na nidhamu.
Post a Comment