0
Ikulu Dar es salaam
Dar es Salaam. Ikulu imewataka Watanzania kuacha kulichukulia suala la kujiuzulu kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kama jambo la ‘kufa na kupona’, huku ikieleza kuwa waziri huyo mpaka sasa bado ni kiongozi wa Serikali. 

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alisema hatua zilizochukuliwa kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi aliyesimamishwa kazi kupisha uchunguzi haziwezi kuwa sawa na za Profesa Muhongo kwa sababu Maswi ni mtumishi wa Serikali na profesa huyo ni mwanasiasa. 

Rweyemamu alitoa ufafanuzi huo baada ya kubanwa na wanahabari waliotaka kujua sababu za Profesa Muhongo licha ya kuwekwa kiporo na Rais Jakaya Kikwete kutokana na kuhusishwa na kashfa ya uchotwaji wa Sh306 bilioni katika Akaunti ya Tegeta Escrow, bado anafanya shughuli mbalimbali za Serikali, ikiwa ni pamoja na juzi kwenda kuhudhuria mkutano nchini Uswisi. 

“Utaratibu wa kumwajibisha yeye (Muhongo) ni tofauti na wa Maswi. Kama mtakumbuka Bunge lilitoa maazimio yake ambayo bado yanaendelea kutekelezwa. Msilichukulie suala hili kama la kufa na kupona,” alisema Rweyemamu. 

Akizungumzia kauli hiyo, Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika alisema, “Kauli hiyo ya Ikulu inadhihirisha udhaifu wa Rais. Rais alisema anamweka kiporo kwa siku mbili, Ikulu inapaswa kueleza ni kwa nini Rais ameamua kumweka kiporo zaidi ya siku hizo mbili wakati alidai kuwa kuna uchunguzi mdogo tu. 

“Kwa namna wanavyomlinda Muhongo na watuhumiwa wengine, naendelea kutoa wito kwa wabunge wenzangu tusaini hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu kwa kuwa kwa kufanya hivyo, baraza la mawaziri litavunjika na hivyo kiporo cha Muhongo na mizigo mingine ndani ya baraza la mawaziri itaondoka.” 

Katika kikao cha 16 na 17 cha Bunge, Bunge kupitia azimio lake la pili liliazimia kwamba Waziri wa Nishati na Madini, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco wawajibishwe kwa kuishauri mamlaka yao ya uteuzi kutengua uteuzi wao. 

Kati ya wote waliolengwa katika azimio hilo ni Profesa Muhongo pekee ambaye mpaka sasa bado hajawajibishwa na mamlaka yake ya uteuzi. 

Jaji Frederick Werema ambaye alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali alijiuzulu, Maswi alisimamishwa kazi, Profesa Anna Tibaijuka aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi alifutwa kazi huku Bodi ya Tanesco ikiundwa nyingine. 

Rweyemamu alifafanua kuwa maazimio ya Bunge yalieleza wazi kuwa waliotajwa wachunguzwe na mamlaka husika. 

Alisema wananchi wanatakiwa kuwa watulivu wakati hatua mbalimbali zikiendelea kufanywa. 

Alisema waziri huyo anafanya shughuli mbalimbali mikoani na hata wizarani kwa sababu bado ni kiongozi na ataendelea hivyo mpaka itakapoamuliwa vinginevyo.  
SOURCE:: mwananchi

Post a Comment

 
Top