Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola alisema jana kuwa
mtuhumiwa huyo alikamatwa Januari 2, mwaka huu, majira ya saa 8:00
alipokuwa kwenye harakati za kutafuta wateja.
Alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa kwenye mtaa wa Rwegasore wilaya ya
Nyamagana jijini hapa akiwa na noti bandia za Sh elfu tano tano zenye
thamani ya Sh 11,955,000, ambazo alizificha ndani ya kasha dogo la
kuhifadhia glasi na kulivisha mfuko mweusi.
Alisema mtuhumiwa baada ya kukamatwa, askari walikwenda naye nyumbani
kwake Buzuruga kwa ajili ya upekuzi, ambako walifanikiwa kumkuta na
dola bandia za Marekani 244,100 sawa na Sh 414, 970,000 za Tanzania na
fedha bandia za Tanzania Sh 12,000,000 ambazo alizificha kwenye kona
chumbani kwake.
“Mtuhumiwa tulimkamata akiwa na fedha bandia Shilingi 23,955,000 na
dola bandia za Marekani 244,100, kama fedha hizo zote zingekuwa ni
halali zingekuwa na thamani ya Shilingi 438,925,000, endapo zingeingia
kwenye mzunguko zingesababisha madhara makubwa na ni wazi uchumi wa nchi
yetu ungeyumba,” alisema Kamanda huyo.
Aliongeza kuwa walipomfanyia mahojiano, mtuhumiwa alikiri kununua
fedha zote hizo eneo la Isibania nchini Kenya Desemba 22, mwaka jana,
kwa thamani ya Sh milioni nane za Tanzania.
Alisema mtuhumiwa aliingiza fedha hizo bandia nchini kwa ajili ya
kuziuza na kwamba alipanga kuuza Sh 300,000 halali kwa Sh 1,000,000
bandia na dola moja alipanga kuiza kwa Sh 800 ya Tanzania.
Polisi wanaendelea kumhoji ili kubaini na kuuvunja mtandao wote,
unaojihusisha na biashara hiyo haramu. Kamanda Mlowola alitoa rai kwa
wafanyabiashara wa jiji na mkoani hapa kuwa waangalifu wanapofanya
miamala ya fedha za kigeni na pia watilie shaka pale wanapouziwa fedha
za kigeni kwa bei ya chini.
Post a Comment