Hayo yalisemwa jana na Mwanasheria Mkuu wa
Serikali (AG), Jaji Frederick Werema ambaye hata hivyo, alimwambia
mwandishi wetu kwamba kabla ya kura hiyo, “lazima daftari la kudumu la
wapigakura liboreshwe kwanza” ili kuwapa fursa wapigakura wapya ambao
hawamo kwenye daftari hilo.
“Kuboreshwa kwa daftari la wapigakura ni lazima
kwa sababu kuna watu wengi wamefikisha umri wa kupiga kura tangu
tulipofanya uchaguzi mkuu na hawamo kwenye daftari hilo, kwa hiyo
hatuwezi kuwanyima fursa ya kupiga kura kwa sababu ni haki yao
kikatiba,” alisema Jaji Werema na kuongeza:
“Lakini lazima tujue pia kwamba kuboreshwa kwa
daftari hilo kunahitaji fedha, kwa hiyo kuboreshwa kwake kutategemea
kama Serikali itatoa fedha kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili kazi
hiyo iweze kufanyika, tusipoboresha daftari tutasababisha kelele na
malalamiko mengi”.
Msimamo wa Jaji Werema ni sawa na ule wa
Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva ambaye amesisitiza mara kadhaa
kwamba tume yake haitoandaa uchaguzi wowote pasipo daftari la kudumu la
wapigakura kuandikwa upya.
Jaji Werema alisema ikiwa Serikali itatoa fedha,
uboreshaji wa daftari unaweza kukamilika ifikapo Februari 2015 na kwamba
inatarajiwa kwamba Machi 30, mwakani kura ya maoni itapigwa kama kila
kitu kitakwenda kama kilivyopangwa.
Alisema upigaji kura utatanguliwa na kampeni
ambazo zitafanyika kwa siku 30 kuanzia mwanzoni mwa Machi ili kushawishi
Katiba inayopendekezwa iungwe mkono au kinyume chake kwa makundi
yanayoipinga.
Hadi sasa gharama za kusimamia kura ya maoni kwa ajili ya kupitisha Katiba Inayopendekezwa zimeendelea kuwa kitendawili.
Jana, Jaji Lubuva alisema asingeweza kuzizungumzia
kwa kuwa yuko Dodoma kikazi na kuelekeza taarifa hizo zinaweza
kupatikana kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi, Julius Malaba.
Hata hivyo, alipotafutwa Malaba alisema anaweza
kuzungumzia suala hilo katika mkutano na waandishi wa habari anaotarajia
kuuitisha wiki hii.
“Wiki hii nitaitisha mkutano na waandishi wa
habari kuhusu daftari la wapigakura. Nadhani itakuwa vyema suala hilo
likiibuliwa kupitia mkutano huo ndipo majibu yanapoweza kupatikana,”
alisema.
Marekebisho ya sheria
Jaji Werema alisema ili kuwezesha utekelezaji wa kura ya maoni,
Sheria ya Kura ya Maoni ya 2013 itapelekwa katika kikao kijacho cha
Bunge kufanyiwa marekebisho.
“Katika kuwezesha hayo, tutaipeleka sheria katika
kikao kijacho cha Bunge ili kufanyia kazi baadhi ya masuala ya kiufundi
kwa lengo la kuwezesha kura hiyo kufanyika,” alisema.
Bunge la Muungano linatarajiwa kuanza mkutano wake
wa Novemba 5. Hata hivyo, Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel alisema jana
kwamba ofisi yake ilikuwa haijapokea taarifa kutoka serikalini kuhusu
marekebisho ya sheria hiyo.
“Bado sijapokea taarifa yoyote kuhusu kusudio hilo
ila kama marekebisho hayo yanatakiwa kufanywa basi wakiyaleta
tutayapokea na kama ni hivyo lazima itakuwa chini ya hati ya dharura,”
alisema Joel.
Sheria ya Kura ya Maoni ya 2013 katika sehemu ya
pili inamtaka Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa kushauriana na Rais wa
Zanzibar, ndani ya siku 14 baada ya kupokea Katiba Inayopendekezwa, kwa
amri itakayochapishwa kwenye Gazeti la Serikali, kuielekeza NEC
kuendesha kura ya Maoni
Amri ya kuitisha kura ya maoni imeainishwa katika
fomu namba moja ya jedwali la kwanza la sheria husika ikimwelekeza Rais
kuainisha Katiba Inayopendekezwa itakayoamuliwa, muda utakaotumika kwa
ajili ya kampeni ya kura ya maoni na kipindi ambacho kura hiyo
itafanyika.
Kwa kuzingatia maelekezo hayo ya kisheria, Rais
Kikwete anapaswa kutoa maelekezo kwa NEC kuhusu kura ya maoni si zaidi
ya kesho Oktoba 22, mwaka huu ambayo ni siku ya 14 tangu alipokabidhiwa
Katiba Inayopendekezwa Oktoba 8 mjini Dodoma.
Makubaliano na TCD
Uamuzi kuhusu kufanyika kura ya maoni mwakani,
umekuja kukiwa na makubaliano baina ya Rais Kikwete na vyama vya
upinzani kupitia Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) ambayo yalifikiwa
Septemba 9, mwaka huu.
Mwenyekiti wa TCD, John Cheyo alipozungumza na
waandishi wa habari mjini Dodoma alisema walikuwa wamekubaliana kwamba
kura ya maoni ifanyike mwaka 2016 ili kutoa fursa ya kufanyika kwa
marekebisho kadhaa katika Katiba ya sasa kwa ajili ya kuwezesha uchaguzi
mkuu wa mwakani.
Hata hivyo, jana Werema alisema mchakato wa Katiba
Mpya kwa mujibu wa makubaliano hayo, ungesimama tu iwapo theluthi mbili
isingepatikana ndani ya Bunge Maalumu.
“Sasa theluthi mbili imepatikana pande zote za Muungano kwa hiyo kwa mujibu wa sheria lazima mchakato uendelee,” alisema Werema.Hata hivyo, alisema hata Katiba Inayopendekezwa ikipitishwa haitaweza
kutumika kwa ajili ya uchaguzi ujao. “Kwa hiyo baada ya kumaliza kura ya
maoni tunaweza kuangalia hayo marekebisho ambayo tunaweza kufanya
kwenye Katiba yetu ya sasa na inaweza kuwa Mei hivi,” alisema.MWANANCHI
Post a Comment