Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, Renatha Mzinga
Kundi la
wananchi wamevamia kituo cha polisi cha Nachingwea mkoani Lindi na kwa
Mkuu wa Wilaya hiyo, Regina Chonjo kulalamikia askari wa jeshi hilo na
serikali kushindwa kuwasaidia ndugu zao wa kike dhidi ya vitendo vya
kinyama, ikiwamo kubakwa, kuuawa na kunyofolewa sehemu za siri.
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Lindi, Renatha Mzinga, amethibitisha kuwapo na matukio
hayo na kukanushwa maiti zote kukutwa zimenyofolewa sehemu za siri.
Hatua ya
wakazi hao ilikuja baada ya mwanamke aliyekuwa mkazi wa Mtaa wa Mianzini
kukuta ameuawa na watu bado hawajafahamika na mwili wake kutupwa katika
eneo la nyumba mpya ya wageni inayopo jirani na inayoendelea nyinghine
inayoendelea kujengwa.
Inadaiwa kuwa mwanamke huyo ni wa nne kuuawa wilayani humo tangu Mei, mwaka huu.
Habari hizo
zinaeleza kuwa kabla ya kumuua, wauaji walimlaza chali, huku wakiwa
wamemvua nguo zote na kubaki utupu na kisha kumbaka.
Hali hiyo
iliibua hasira kutoka kwa wananchi hao, ambao waliamua kufanya
maandamano na kuzingira kituo hicho cha polisi na nyumbani kwa mkuu huyo
wa wilaya.
Mmoja wa
wananchi hao alidai kuwa walifikia hatua hiyo ili kuwasilisha
malalamiko yao kutokana na kukithiri kwa vitendo hivyo vya kinyama bila
vyombo vya usalama wala serikali kuwakamata watuhumiwa.
Aliitaja sababu nyingine kuwa ni kutokana na mwili wa marehemu huyo kuchelewa kuondolewa katika eneo ulikotupwa.
Wakati baadhi ya wananchi hao wakimbia nyumbani kwa kwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Regina Chonjo, lakini hawakufanikiwa kumkuta.
Inaelezwa
kuwa Chonjo alikuwa safarini mjini Lindi kuhudhuria kikao cha maandalizi
ya maonesho ya ya kilimo maarufu kama Nanenane, ambayo kitaifa mwaka
huu yanafanyika mkoani Lindi.
Chonjo alipoulizwa na NIPASHE, alithibitisha kuwapo kwa vurugu hizo, lakini hakuwa tayari kuzungumza kwa kirefu.
“Ni kweli
vurugu hizo zimetokea, lakini nashindwa kuzielezea zaidi, kwani na mimi
nimepata taarifa hii nilishaondoka kuja hapa Lindi kuhudhuria kikao cha
Nanenane,” alisema Chonjo.
Alisema kutokana na tukio hilo, amelazimika kukatisha kuendelea na kikao hicho na kurejea Nachingwea.
Wakizungumza
na NIPASHE kwa nyakati tofauti jana, wakazi hao walidai kuwa ndugu zao,
ambao ni wasichana wenye umri chini ya miaka 30, wamekuwa wakifanyiwa
unyama huo na kwamba, hadi kufikia jana, wanane walikuwa wamekwishauawa.
“Tumechoshwa
sisi. Kila kukicha unakuta msichana mmoja kafa, huku wamemkata maumbile
yake ya sehemu za siri na...,” alidai kwa uchungu mmoja wao.
Aliongeza: “Tumeishalalamika kwa Jeshi la Polisi. Mpaka sasa wanaofanya vitendo hivyo bado hawajakamatwa.”
Walidai mwaka jana waliuawa wasichana wawili na kwamba, ndani ya mwezi huu watano.
Wakazi hao walidai alfajiri jana, aliuawa mwanamke huyo ambaye ameacha mtoto mchanga na watu hao wasiojulikana.
Walidai
kinachowaumiza ni mauaji hayo kufanyika, lakini polisi hawawapi
ushirikiano na ndiyo maana wamelazimika kuvamia kituo hicho na nyumbani
kwa mkuu wao wa wilaya.
Katibu wa
Chama cha ADC Wilaya ya Lindi, Moshi Mataka alisema wamechoshwa na
matukio hayo.Alisema wamelalamika, lakini mpaka sasa hakuna
kinachoendelea juu ya kuwachukulia hatua watuhumiwa.
Mataka
alisema wameanza kufanya vikao kuelimishana na wananchi juu ya kupambana
na watu hao, ambao wanawafanyia wasichana vitendo vibaya.
“Tunataka kuandaa ulinzi shirikishi ili kudhibiti hali hii, ambayo imekuwa inajitokeza kila mara,” alisema Mataka.
Mchukua Kumbukumbu za Wilaya hiyo, Shakili Bhimi alisema wanawake 10 wameuawa kwa kubakwa na kunyofolewa sehemu zao za siri.
Alisema
pamoja na kunyofoa sehemu za siri, pia wanawanyofoa vitu vya uzazi kwa
ajili ya kuvipelekwa kwa waganga wa jadi kupata madini ya dhahabu kwa
wingi.
“Mwaka jana
waliuawa wasichana wawili na mwaka huu wameuawa wasichana nane na idadi
hiyo inakuwa ni jumla ya wasichana 10,” alisema Bhimi.
Akizumgumzia
kuhusu wananchi kukosa ushirikiano wa polisi, Kamanda Mzinga alikanusha
akisema wao ndiyo wanaokosa ushirikiano wao.
“Unajua
hivyo ni visasi vinatoka kwa hao hao wananchi. Kama mtu kaolewa na
kuachana na mumewe na kuolewa kwingine, ndio hivyo. Mtu aliyeachwa
anamvizia msichana na kufanya mauaji hayo. Hili sisi tulilijua baada ya
kuwakamata mwaka jana watu wawili na kuwahoji,” alisema Kamishna
Msaidizi Mzinga.
Alisema
mwaka jana waliuawa wasichana wawili na walipowahoji wananchi ndipo
walipopata ushirikiano wa kuwakamata watuhumiwa, ambao alisema mpaka
sasa wapo makahamani wana kesi za kujibu.
Pia
alikanusha maiti wote wanaokutwa wanakuwa wamekatwa sehemu za
siri.Alisema maiti wengi wamekuwa wakibakwa na ni mmoja tu wa juzi ndiye
alikutwa akiwa amekatwa sehemu za siri huku ikiwa zikiwa zimetiwa miti.
Pia alisema
walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi waliovamia
kituo hicho na kwamba, hakuna mali yoyote katika ofisi hiyo
iliyoharibika wala raia aliyepata majeraha katika tukio hilo.
Alisema mpaka sasa ni watu saba waliouawa katika vitendo hivyo vya kinyama, wakiwamo wawili mwaka jana, watano mwaka huu.
Hata hivyo,
alisema polisi wameanza kuingia katika maeneo mbalimbali ya vijiji
kuwasaka na kuwakamata waliohusika na mauaji hayo.
SOURCE: NIPASHE
Post a Comment