Mwenyekiti
wa CUF Taifa Prof. Ibrahim Lipumba, akiunga mkono moja ya hoja za
marekebisho ya katiba ya CUF yaliyofanywa katika ukumbi la Ubungo Plaza
Dar es Salaam.
Na Hassan Hamad (OMKR).
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CUF Taifa wamepitisha mapendekezo mbali
mbali yaliyowasilishwa na Baraza Kuu la uongozi la chama hicho kuhusu
marekebisho ya baadhi ya vipengele vya katiba ya chama hicho.
Katika
mkutano mkuu wa chama hicho unaoendelea kwa siku ya tatu katika ukumbi
wa Ubungo Plaza Dar es Salaam, wajumbe hao pamoja na mambo mengine
wamekubaliana kuwa mkutano mkuu wa chama hicho ufanyike mara moja katika
kipindi cha miaka mitano badala ya miaka miwili na nusu kama
ilivyopitishwa na mkutano mkuu mwaka 2009.
Katibu Mkuu wa chama hicho Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema
hatua hiyo imefikiwa baada ya kuona kuwa mapendekezo yaliyopitishwa
mwaka 2009 hayatekelezeki kutokana na ukosefu wa fedha unaokikabili
chama hicho.
Hata hivyo amesema kwa mujibu wa sheria hiyo mkutano mkuu taifa unaweza kufanyika kwa dharura wakati wowote utakapohitajika.
Wajumbe
wa mkutano huo pia wamekubali mapendekezo ya kuongezwa ngazi ya uongozi
ya Jimbo kwa upande wa Tanzania Bara ambapo kabla ya hapo hawakuwa na
ngazi hiyo.
Mapendekezo
mengine yaliyopitishwa ni kwa Mwenyekiti wa chama hicho kupewa uwezo wa
kuongeza wigo wa uteuzi kwa wajumbe wa kamati tendaji taifa, nje ya
wajumbe wa baraza kuu na mkutano mkuu kwa kadri anavyoona inafaa kwa
maslahi ya chama.
Aidha wajumbe hao wamekubaliana kuwepo kamati ya nidhamu na maadili
kikatiba katika ngazi zote za uongozi kuanzia ngazi ya tawi hadi taifa,
sambamba na mambo ya uchaguzi kuondolea kwenye katiba na badala yake
yabakie kwenye kanuni.
Kwa upande mwengine wajumbe wa mkutano huo wamekataa pendekezo la
kuwepo uongozi katika ngazi ya Mkoa kwa upande wa Tanzania Bara, na
kutaka ngazi za uongozi ziendelee kama kawaida kwa kuwepo ngazi ya
Wilaya ikifuatiwa na ngazi ya Taifa.
Wajumbe hao wamekataa pendekezo hilo kwa madai kuwa ngazi hiyo
itaongeza utitiri wa viongozi wasiokuwa na ulazima kwa maendeleo ya
chama.
Pendekezo jengine walilolikataa ni uteuzi wa makatibu wa Wilaya
ambapo wamekubaliana kuwa makatibu wa ngazi hiyo waendelee kuchaguliwa
na wajumbe wa mkutano mkuu wa Wilaya.
Marekebisho
ya katiba hiyo yakayoingizwa kwenye “Katiba ya CUF ya mwaka 1992 toleo
la 2014”, yataanza kutumika kuanzia tarehe 22/08/2014.
Wajumbe
wa Mkutano Mkuu wa CUF Taifa wakiunga mkono moja ya hoja za marekebisho
ya katiba ya CUF yaliyofanywa katika ukumbi la Ubungo Plaza Dar es
Salaam.
chanzo:eddy.
Post a Comment