0



Na. Jeshi la Polisi. 

Michezo ya kuwania kombe la Sirro Kibiti mwaka 2018 inatarajiwa kuzinduliwa jumatatu Mei 7 na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro katika uwanja wa Samora Wilayani Kibiti.

Akizungumza wilayani Kibiti baada ya kukagua maandalizi hayo, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi wa Polisi Barnabas Mwakalukwa amesema uzinduzi huo utahudhuriwa pia na Viongozi mbalimbali kutoka mkoa wa Pwani. 

Mwakalukwa amesema lengo la michezo hiyo ni kuwaweka pamoja na kudumisha usalama kwa wakazi wa Wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji baada ya matatizo yaliyowakumba kumalizika. 

Ametoa wito kwa wakazi wa maeneo hayo kujitokeza kwa wingi ili kushuhudia burudani mbalimbali pamoja na maneno ya viongozi mbalimbali yatakayotolewa katika ufunguzi wa michezo hiyo ambapo ratiba itaanza saa saa nne asubuhi. 

Kwa upande wake Mratibu wa Kombe hilo, Koplo Ramadhan Tamimu amesema michezo hiyo itakapofikia tamati bingwa atajinyakulia kombe na fedha taslimu Milioni moja huku yakichagizwa na kauli mbiu ya “Kibiti Salama, Jamii Salama” 

Naye Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Kibiti Rashid Mkinga amesema wamejiandaa vyema na anauhakika wa kombe hilo kubaki wilayani Kibiti kwa kuwa pamoja na kuwa na timu bora lakini pia wanatarajia kupata mashabiki wengi. 

Ufunguzi huo utapambwa na burudani mbalimbali zikiongozwa na Bendi ya dansi ya Jeshi la Polisi, Msanii wa nyimbo za asili Ndolela, Man Prince na vikundi mbalimbali kutoka Wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji.

Post a Comment

 
Top