0

Serikali ya awamu ya tano kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imesema haina mpango wowote kwa sasa kutoa elimu bure kwa ngazi ya kidato cha tano na sita nchini bali wamejipanga katika kuboresha miundombinu pamoja na kutoa elimu iliyo kuwa bora.


Kauli hiyo imetolewa leo Mei 09, 2018 na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. William Ole-Nasha Bungeni Jijini Dodoma kwenye kikao cha 25 mkutano wa 11 wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge Edwin Mgante Sanda aliyetaka kujua ni lini serikali itatekeleza suala la elimu bure kwa kidato cha tano na sita ambalo ni kundi pekee lililobaki kugharamiwa na serikali.


"Serikali imeweka kipaumbele cha kuhakikisha fursa sawa ya kutoa elimu kwa ngazi ya awali 'msingi na sekondari' kwa sababu hii ndio ngazi ya elimu ambayo humpatia muhusika stadi za msingi ambazo ataweza kukabiriana na mazingira yake. Dhana ya elimu bila malipo inazingatia uendeshaji wa shule bila ya ada wala michango ya aina yeyote ya lazima kutoka kwa wazazi au walezi", amesema Ole-Nasha.


Pamoja na hayo, Ole-Nasha ameendelea kwa kusema "kwa sasa serikali haijaandaa mpango wa elimu bure 'bila malipo' kwa ngazi ya kidato cha tano na sita bali inaelekeza jitihada zake za kuboresha miundombinu na ubora wa elimu kwa ngazi zote za elimu nchini ikiwemo elimu ya kidato cha tano na sita".


Kwa upande mwingine, Naibu Waziri Ole-Nasha amesema mpango wa elimu bila ya malipo nchini kutoka shule ya msingi hadi sekondari umeweza kuonesha mafanikio makubwa katika sekta ya elimu tangu ulipoanza mwaka 2016.

Post a Comment

 
Top