Mabingwa wapya wa ligi kuu ya England kwa msimu wa 2017 - 2018, klabu ya Manchester City imekabidhiwa kombe la ubingwa wa ligi kuu ya England licha ya kukubali sare ya bila kufungana na Huddersfield Town.
Mabingwa hao wakicheza ugenini katika dimba la Kirklees wamefikisha jumla ya alama 94 katika michezo 36 waliyocheza msimu huu na wakisaliwa na michezo miwili kabla ya ligi kumalizika jumapili ijayo.
Kama ilivyo kawaida wachezaji wa Huddersfield walijipanga pande mbili kabla ya mchezo kuanza na kuwapigia makofi mabingwa hao wapya wa Epl na ukiwa ni ubingwa wao wa tatu katika kipindi cha miaka saba.
City watakuwa wenyeji wa Brighton katika dimba lao la Etihad siku ya jumatano ya tarehe 9 kabla ya kumaliza ligi Mei 13, kwa kusafiri kwenda kucheza na Southampton mchezo ukicheza katika dimba la St Marys.
Meneja wa Arsenal Arsene Wenger, akisimama katika bechi la Arsenal kwa mara ya mwisho katika dimba lao la Emirates alishuhudia timu yake ikiibuka na ushindi wa kishindo wa magoli 5-0 dhidi ya Burnley.
Magoli ya Arsenal yalifungwa na Pierre-Emerick Aubameyang aliyefunga magoli mawili, Mfaransa Alexandre Lacazette akafunga goli moja na magoli mengnine yakifungwa na Sead Kolasinac na Alex Iwobi.
Arsenal watacheza mchezo wao wa mwisho wa kumaliza ligi ugenini kwa kuikabili klabu ya Huddersfield Town, na mchezo huo ndio utakuwa mchezo wa mwisho wa meneja Arsene Wenger ambae amedumu katika klabu hiyo kwa miaka 22.
Chelsea wakicheza katika dimba lao la Stanford Bridge waliibuka kidedea kwa ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Liverpool na hivyo kuweka hai matumaini yao ya kuweza kumaliza katika nafasi nne za juu na kucheza michuano ya klabu bingwa ulaya msimu ujao
Chelsea wenye alama 69, walipata goli lao kupitia kwa mshambuliaji Olivier Giroud, The Blues wamesaliwa na michezo miwili jumatano ya tarehe 9 watacheza na Huddersfield Town na watamaliza ligi kwa kucheza na Newcastle United.
Majogoo wa Anfield Liverpool wao wanasalia katika nafasi ya tatu wakiwa na alama 72,na wamesaliwa na mchezo mmoja utakaopigwa jumapili ya Mei 13,dhidi ya Brighton siku ambayo msimu wa 2017/2018 utakuwa unamalizika.
Post a Comment