Kiongozi wa Kamati ya Majadiliano kwa upande wa Serikali, Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi akitia saini pamoja na Mkurugenzi wa Tanzanite One Faisal Juma mara baada ya kufikia makubaliano na Kampuni hiyo ya Uchimbaji wa Madini ambayo imekubali kulipa fidia kwa Serikali pamoja na mambo mengine ya Kimkataba.
Kiongozi wa Kamati ya Majadiliano kwa upande wa Serikali Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi akibadilishana hati za Makubaliano na Mkurugenzi wa Tanzanite One Faisal Juma mara baada ya Kampuni hiyo ya Uchimbaji wa Madini kukubali kulipa fidia kwa Serikali.
Kiongozi wa Kamati ya Majadiliano kwa upande wa Serikali Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi akiwa na watendaji wa Kampuni ya Uchimbaji madini ya Tanzanite One wakati akielekea kusaini hati za makubaliano baina ya kampuni hiyo na Serikali.
Kiongozi wa Kamati ya Majadiliano kwa upande wa Serikali Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi akizungumza mara baada ya kuhitimisha mazungumzo na kusaini hati ya Makubaliano yatakayoiwezesha Serikali kulipwa fidia na Kampuni ya uchimbaji madini ya Tanzaniate.
Kiongozi wa Kamati ya Majadiliano kwa upande Kampuni ya Tanzanite One Faisal Juma akizungumza mara baada ya kuhitimisha mazungumzo na kusaini hati ya Makubaliano yatakayoiwezesha Serikali kulipwa fidia na Kampuni ya uchimbaji madini ya Tanzaniate.
Kiongozi wa Kamati ya Majadiliano kwa upande wa Serikali Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi akiagana na Mkurugenzi wa Tanzanite One Faisal Juma mara baada ya Kampuni hiyo ya Uchimbaji wa Madini kukubali kulipa fidia kwa Serikali pamoja na mambo mengine ya Kimkataba kama walivyokubaliana. PICHA NA IKULU
********************************************
Kampuni ya uchimbaji madini ya Tanzanite One imekubali kuilipa Serikali fidia pamoja na kodi watakayokubaliana kutokana na dosari zilizokuwepo hapo awali.
Makubaliano hayo yametiwa saini Jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kamati iliyoundwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli Profesa Palamagamba Kabuni na Mkurugenzi wa Tanzanite One Bw.Faisal Juma.
Akizungumza mara baada ya kutia saini makubaliano hayo, Mwenyekiti wa kamati ya majadiliano kwa upande wa Serikali, Prof. Palamagamba Kabudi amesema Tanzanite One imekubali kulipa fidia Serikali kutokana na mambo iliyofanya ambayo yalikuwa kinyume na utaratibu ulioleta hasara kwa Serikali.
Amesema fidia hiyo inatakiwa kulipwa kwa awamu ambapo awamu ya kwanza italipwa ndani ya wiki mbili kuanzia leo na haitahusisha Kodi. Pia Kampuni hiyo Tanzanite One italazimika kulipa kodi kama kawaida inazodaiwa na Serikali na tozo nyingine zote zinazodaiwa na Serikali.
Pia Serikali imekubaliana na Kampuni ya Tanzanite One kuwa itafuata masharti yote ya sheria ya madini ya mwaka 2010 ambayo inaeleza kuwa ni Watanzania tu ndio wanaoruhusiwa kuchimba madini ya Vito na pale ambapo watanzania hawana uwezo huo ndipo wanapoweza kuingia ubia na wageni.
Aidha Prof. Kabudi amesema kuhusu wachimbaji wadogo wadogo wa Tanzanite katika eneo la Mirerani utaratibu mpya unawekwa lengo kubwa ikiwa ni kutekeleza sheria ya madini ya mwaka 2010 ambayo inalenga madini ya vito kuwa mikononi mwa Watanzania.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Tanzanite One Faisal Juma amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuunda kamati hiyo ya kizalendo katika kufuatilia rasilimali za madini nchini ambapo wameweza kujadiliana na kufikia muafaka wa kulipa fidia ikiwa ni mbali na malipo yote yaliyotakiwa kulipwa serikali ikiwemo kodi.
Amesema Tanzanite One itahakikisha inafuata taratibu zote za Sheria ya Madini ya mwaka 2010 kwa lengo la kuhakikisha rasilimali ya madini inawanufaisha Watanzania na kwamba uvunjifu wa sheria uliofanywa na kampuni hiyo hautajirudia tena.
“Sisi kama Tanzanite One tunaihakikishia Serikali kuwa uaminifu uliotuonyesha na sisi pia kama Kampuni tutahakikisha tunakuwa waaminifu na kuwa zao hili linanufaisha taifa kutokana na imani aliyotuonyesha Mhe. Rais kama wananchi wake kutupa nafasi na fursa ya kusikilizwa ili kurekebisha makosa tuliyoyatenda” amesema Faisal.
Faisal amesema Tanzanite One itahakikisha haitafanya makosa iliyofanya mara ya kwanza na hivyo kuwa mfano wa kampuni nyingine za madini kuhakikisha rasilimali za madini zinawanufaisha Watanzania.
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi Mawasiliano ya Rais, IKULU.
Dar es Salaam
16 Mei, 2018
Post a Comment