Kiungo wa kati wa Manchester United Paul Pogba amesema hana tatizo na meneja Jose Mourinho na hafikirii kuihama klabu hiyo. Hii ni licha ya Mfaransa huyo wa miaka 25 kuwa akiwekwa benchi mechi za karibuni. (Telefoot kupitia Manchester Evening News)
Everton, West Ham na Swansea wote wanamtaka mshambuliaji wa Mali anayechezea Porto Moussa Marega, 26. (Mirror)
Meneja wa zamani wa Chelsea Gianluca Vialli amesema meneja wa sasa wa klabu hiyo Antonio Conte bila shaka anasubiri sana kuondoka. (Sky Italia kupitia Metro)
Conte anasema hana wasiwasi kuhusu mustakanali wake kama meneja Chelsea baada ya klabu hiyo kulazwa 3-1 na Tottenham na kudidimiza matumaini ya klabu hiyo kufuzu kwa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya msimu ujao. (Guardian)
Taarifa zinazomhusisha fowadi wa Brazil mwenye miaka 26 Neymar na kuhamia Real Madrid ni "uvumi usio na msingi" kwa mujibu wa mchezaji mwenzake Paris St-Germain Kylian Mbappe. (Telefoot via Goal)
Beki wa miaka 24 kutoka Ufaransa anayechezea Barcelona Samuel Umtiti ambaye amehusishwa na kuhamia Manchester United, anasema hali kwamba kifungu cha kumfungua kutoka kwa mkataba wake klabu hiyo si cha juu sana inamtia wasiwasi. Hata hivyo, amesema ametosheka kusalia katika klabu hiyo. (Express)
Manchester City wanakabiliwa na ushindani kutoka kwa Borussia Dortmund, Feyenoord na PSV Eindhoven katika kutafuta saini ya kinda wa miaka 18 anayechezea Fenerbahce Eljif Elmas ambaye anatokea Macedonia. (Bild - kwa Kijerumani)
Roma wamesema kufikia sasa bado hawajapokea ofa zozote za klabu zinazomtaka kipa Mbrazil Alisson, 25, na kwamba hawana nia yoyote ya kumuuza. Hayo ni kwa mujibu wa mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo ya Italia Monchi. Alisson amehusishwa na kuhamia Liverpool. (Mediaset Premium kupitia Football Italia)
West Ham watalazimika kuwalipa Sporting Lisbon jumla ya euro 30m (£27m) iwapo wanataka kumnunua mchezaji Rodrigo Battaglia, 26, kutoka Argentina ambaye pia anatafutwa na klabu tatu za Italia: Inter Milan, Roma na Napoli. (O Jogo - kwa Kireno)
Meneja wa West Ham David Moyes ameashiria kwamba bado hajaamua kuhusu iwapo watataka kubadilisha uhamisho wa mkopo wa kiungo wa kati wa miaka 25 Joao Mario kutoka Inter Milan kuwa wa kudumu. (Times)
Kipa wa Crystal Palace, 31, Wayne Hennessey ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu angependa kusalia Selhurst Park. (Croydon Advertiser)
Sunderland wanamtaka kipa wa miaka 24 anayechezea Reading Jonathan Bond, ambaye mkataba wake wa sasa unafikia kikomo mwisho wa msimu. (Newcastle Chronicle)
Mshambuliaji wa Manchester City Sergio Aguero atakuwa amepata nafuu vya kutosha kuweza kuwa kwenye benchi mechi ya mkondo wa kwanza robofainali Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Liverpool. (Star)
Mkuu wa zamani wa waamuzi Keith Hackett amesema mwamuzi Craig Pawson hakutoa uamuzi ufaao kwa visa vilivyowahusisha wachezaji Erik Lamela na Jan Vertonghen katika mechi ambayo Tottenham walishinda 3-1 dhidi ya Chelsea. Anaamini iwapo video ingetumiwa, Spurs wangemaliza mechi na wachezaji tisa. (Telegraph)
Meneja wa Stoke Paul Lambert anataka teknolojia ya video (VAR) ianze kutumiwa katika Ligi ya Premia baada ya klabu hiyo kuadhibiwa kwa mkwaju wa penalti ambao ulizalisha bao la kwanza mechi yao dhidi ya Arsenal. Arsenal walishinda 3-0 uwanjani Emirates. (Mail)
Lakini mshambuliaji wa Monaco Radamel Falcao anaamini VAR "itaua soka" baada ya klabu yake kushindwa katika fainali ya Kombe la Ligi Ufaransa na Paris St-Germain. (Marca)
Meneja wa Manchester United Jose Mourinho ametetea uchezaji wa klabu yake msimu huu, ambapo wamo nafasi ya pili msimu huu, kwa kuwaambia kwamba "nyote mnasema walio nafasi ya tatu, nne, tano na sita ni bora kuliko sisi, lakini si kweli kwani tuna alama nyingi kuwashinda". (Mirror)
Meneja wa Huddersfield David Wagner anasema klabu yake ina kila wanalohitaji kuhakikisha wananusurika Ligi ya Premia mwisho wa msimu. (Huddersfield Examiner)
Kiungo wa kati wa Manchester City Kevin de Bruyne amesema wachezaji wa klabu hiyo wana hamu sana ya kutwaa taji la Ligi ya Premia kwa ushindi wa "kihistoria" dhidi ya mahasimu wao wa jiji Manchester United katika debi Jumamosi. (Independent)
Mshambuliaji wa Bournemouth Jermain Defoe amedai kwamba anaweza kuishindia England Kombe la Dunia iwapo mkufunzi wa timu ya taifa England Gareth Southgate atamchagua mchezaji huyo kwenda kucheza Urusi. (Telegraph)
Beki wa Marekani na Fulham Tim Ream anaamini kwamba wachezaji wa Marekani hubaguliwa katika soka Uingereza. (Times)
Post a Comment