0


Na; Raidhani Mohamedi, Liwale - Lindi Tz

      Leo nianze kwa kuwapongeza Wanawake wote Tanazania kwa kuungana na Wanawake wenzao Ulimwenguni kote kusherehekea Siku ya Wanawake Duniani, Sherehe zilizofanyika Juzi kwenye maeneo mbalimbali Ulimwenguni

Kwa hapa Liwale najuwa Wanawake wote walikutana pale kwenye Uwanja wa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale wakiongozwa na Mh.Amida Abdallah, Mbunge wa Viti maalumu kupitia Chama cha Mapinduzi {CCM}, na kwa Mama zangu na Dada Zangu walioko ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Lindi nimepata taarifa kuwa waliujaza kikamilifu Uwanja wa Michezo wa Mpilipili wakishuhudia tukio la kihistoria la kupatikana mshindi wa shindano maalumu la 'Ahsante kwa kunipenda' lililoratibiwa na kuendeshwa na Mashujaa FM radio, Kituo cha utangazaji kinachopatikana Mkoani hapa, Hongereni sana.

Nichukue fursa hii kutoa nasaha zangu kwa Wanawake wote Duniani hasa Wanawake wakitanzania, mtumie Sikukuu hii kwa kujitafakari na kutengeneza mipango kazi ambayo itawafanya muwe wa tofauti zaidi na hatimaye tuwaone mkiongezeka katika nyanja mbalimbali za Kisiasa, Kijamii, Kiuchumi nk, na si kuongezeka tu bali kuongezeka kwa manufaa yenu binafsi na Taifa kwa ujumla, Ahsante sana Mama; Ahsante Kwa Kunipenda.

Hoja yangu kubwa ambayo nataka niizungumze leo inawahusu saana Wanasiasa, Najuwa nikitaja Wanasiasa kwa haraka mtazamo ulio wa wengi wataelekeza kwa Waheshimiwa Madiwani na Wabunge pekee kwani hawa ndio mara nyingi zinapofika hoja za kisiasa katika Jamii ndio wamekuwa walalamikiwaji wakubwa, Sasa nataka niwaambie kuwa licha ya hao Madiwani na Wabunge, Wakuu wa Wilaya na Mikoa, Mawazir na Manaibu Mawaziri, Wenyeviti wa Serikali za Vijiji, Mitaa, Halmashauri, Shehia na Wajumbe wao wote ni Wanasiasa

Wengine ambao pia wanajulikana sana kuwa ni Wanasiasa ni Viongozi wenyewe wa Vyama vya Siasa kuanzia Mashina, Matawi hadi Taifa bila kusahau Viongozi Wakuu wa Serikali yaani Rais na Makamu wa Rais nao pia ni Wanasiasa, ndio maana hata wakati wa kuwatafuta watumishi hewa ndani ya nchi hii Viongozi hao hawakuguswa kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa wakati ule na aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora {Sasa ni Waziri wa Madini} Mh.Angela Kairuki.

Abraham Lincon, aliyekuwa Rais wa 16 wa Marekani aliwahi kutoa kauli isemayo kuwa ''Democracy is the government of the people, by the people, for the people'', kauli ambayo inaendelea kuishi hadi sasa ambapo alichambua kwakina maana na tafsiri halisi ya neno 'Demokrasia', Sitaki kumnukuu sana na kupita kwenye njia za Abraham Lincon kwenye makala yangu hii lakini ninachotaka kusema ni kwamba Siasa, Demokrasia na Utawala Bora ni maneno ya aina tofauti kimatamko lakini kiutendaji ni maneno yanayoshabihiana kwenye baadhi ya nyanja.

Tanzania ni nchi ya kidemokrasia kama yalivyo mataifa mengine Afrika na Ulimwenguni, Tanzania tuna kila sifa zinazotazamwa na mataifa yaliyo mengi ya ndani na nje ya Afrika lakini ni ukweli usiofichika kuwa makosa tunayoyaona madogo kwasasa huenda yakaja kuharibu sifa ya Taifa letu pendwa siku za usoni, moja ya sifa ya Taifa la kidemokrasia ni kuwa na chaguzi mbalimbali za kisiasa ambazo Vyama vingi vya siasa husimamisha watu wao wanaowaamini yaani Wagombea kisha Wananchi husika hufanya maamuzi ya yule wanayemhitaji kuwa Kiongozi wao kwa wakati huo kufuatia sera alizozinadi wakati wa kampeni zake bila kujali chama cha siasa alichotoka, muhimu ni kuchaguliwa kihalali.

Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, Uchaguzi Mkuu hufanyika kila baada ya Miaka mitano ambapo huusiisha Madiwani, Wabunge na Rais, kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ukiacha hao pia huchagua Rais wa Serikali ya Mapinduzi, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi nk

Kilichonifanya kuandika hapa Makala hii ni kutokana na 'chuki' 'zinazotengenezwa' na 'kuonekana' kila uchwao miongoni mwa Wanasiasa hao. Kuna wakati watu walijiuliza maswali mengi sana kufuatia kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Amos Makala ambapo alitangaza kumuomba msamaha Rais Magufuli eti kwakuwa Mgombea Udiwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo {Chadema} aliibuka kidedea kwenye Uchaguzi wa marudio uliofanyika Mkoani humo.

Wakati ukistaajabu ya Makala, nakuletea yanayoendelea kufanywa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Mashaka Gambo ambapo mara kadhaa ameonekana kwenye majukwaa ya Kisiasa hasa yale ya Chama tawala akinadi Wagombea wa Chama hicho kwenye Chaguzi mbalimbali.

Hiyo ni baadhi tu ya mifano lakini yapo mengi sana ambayo yamekuwa yakifanywa au kuzungumzwa na Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na hata Wakurugenzi watendaji wa Halmashauri zetu, na Viongozi wengine wa Kada tofauti na wenye nyazfa za kuheshimika ndani ya Serikali ambapo mara kadhaa wamejihusisha na masuala ya kisiasa, Sio dhambi mtu kushiriki kwenye harakati hizo lakini ni vyema zaidi kujitafakari kwa kina kuhusu nafasi zetu za kiutawala kabla ya kuuingiza 'ushabiki'

Kikatiba Wakuu wa Mikoa na Wilaya ndio Wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama kwenye maeneo yao ya utawala, Kwa tafsiri ya kawaida hawa hawakutakiwa kujionesha kuwa na ushabiki wa chama chochote kile cha Siasa kwani wanaongoza wafuasi wa Vyama vyote kwenye maeneo hayo, Mfano kule Mbeya kwa Amosi Makala au kule Arusha kwa Mrisho Gambo hivi unadhani Viogozi hawa wanatafsiriwaje na Wakina Joseph Mbilinyi 'Sugu' au Godbles Lema ambao kimsingi ni Wabunge wa kuchaguliwa kisheria na Wananachi kupitia Chama cha Upinzani cha Cha Demokrasia na Maendeleo {CHADEMA} ambacho ni 'Mbwa na Kima' na Chama cha Mapinduzi {CCM}, Hivi ni kweli watu hawa wanaweza kukaa 'meza moja' kujadili masuala ya maendeleo kwa Wanachi wanaowaongoza wakati tayari wameuonesha umma kuwa wako na mitazamo tofauti

Hali hii inaathiri zaidi pale Mkuu wa Mkoa au wa Wilaya husika anapofikia maamuzi ya kiutalawa kwa kuamua kumuweka ndani Mbunge, Diwani au Kiongozi yeyote yule wa Kisiasa anayetoka nje ya chama anachodaiwa kushabikia, inawezekana ni kweli mhusika alitakiwa kuwajibishwa kwakuwa alichokifanya kwa wakati huo hakikustahili na kipo kinyume na sheria au taratibu zilizopo lakini ukweli huo unaweza kujificha na jamii ikaangalia 'ukada' wa hao Viongozi 'waliswekana' 'korokoroni', hii si sawa

Wakati natafakari haya ya Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Siku moja nilihudhuria Kikao cha ndani cha chama fulani nikiwa kama mgeni mualikwa nikiiwakilisha taasisi yangu ya kihabari lakini kiukweli nilichokutananacho kule sikuamini macho yangu kumuona Kiongozi kama yule mwenye nyadhfa kubwa Serikalini akishawishi Wasaidizi wake wafanye yale

Alichokuwa akiwaagiza kiufupi ni kwamba Viongozi waliojiona au wanaojitambua kuwa wamewekwa hapo na mtu wa chama fulani basi wakigundulika 'hawakisapoti' chama hicho hata nafasi zao ziko rehani. Swali langu kwanini yule Mheshimiwa aseme vile?, ni kwa maslahi ya nani?, Je hajuwi kuwa yeye mwenyewe na hata hawa Wasaidizi wake ni Viongozi wa Umma/Serikali na si wa chama fulani cha Siasa?, haoni kama kufanya hivyo kunaweza kusababisha sintofahamu siku za usoni?

Lakini hii imekuwa ni Desturi ya Viongozi wengi 'kutojitambua' nafasi walizopo na kutowatambua wale wanaowaongoza, Kuna Siku Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Kasimu Majaliwa alifanya Ziara Mkoani Mbeya na kufanya Mkutano wa hadhara kwenye eneo moja lililopo ndani ya Halmashari ya Jiji la Mbeya, Jiji ambalo linaongozwa na Mstahiki Meya kutokea Chama cha Demokrasia na Maendeleo {CHADEMA} lakini kama hiyo haitoshi Mbunge anayeongoza Jimbo la Mbeya Mjini naye ni Mwanachadema alkadharika hata Madiwani walio wengi ndani ya Halmashauri hiyo ni Chadema, kwa muktadha huo ndio kusema kwamba Chadema imepewa nafasi kubwa sana ya Uongozi ndani ya eneo hilo lakini si kwamba ndio watendaji wa kila kitu

Sasa kwenye Mkutano ule wa Waziri Mkuu Majaliwa uliohudhuriwa na Vongozi wengine mbalimbali wa Serikali na Kisiasa pamoja na Wananachi, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Amos Makala akampatia fursa ya kusalimia Mbunge wa Jimbo hilo Joseph Mbilinyi 'Sugu', baada ya kupanda jukwaani 'Sugu' 'typically' alichokizungumza hapo ni 'usiasa' mtupu.

'Sugu' hakuona haibu wala haya kusema maendeleo ya Jiji hilo yanaenda kwa kasi kwasababu ya kuwa Viongozi wake ni wa upinzani, hii si kweli kwani kama ndio hivyo Mh.Majaliwa alikuwepo pale kwa kazi gani wakati Chadema wapo?, Nina mengi sana ya kuandika kwenye Makala hii kwasababu imefikia hatua sasa Siasa zetu zinaelekezwa hata kwenye mihimili ya Serikali mfano Bunge na Mahakama kitu ambacho ni kinyume na Sheria

Hivi ni mara ngapi watu wamekosoa Bunge letu kuwa halina mvuto na limejaa malumbano na hata wakati mwingne Waheshimiwa Wabunge wenyewe kwa wenyewe kutoleana lugha za dharau na kuudhi ambapo imefikia wakati baadhi ya Wabunge hao hao hupeleka lugha hizo hata kwenye Kiti cha Spika, tumepata taarifa mara ngapi Vikao vingi vya Madiwani kwenye Halmashauri zetu vinaanza vizuri na kuishia pabaya, Je kuhusu Vikao au Mikutano ya ngazi ya Tarafa, Kata au hata Mitaa, Vijiji na Vitongoji?, Yote ni kwa ajili ya Siasa

Professor Ibrahim Hamisi Juma ambaye ni Jaji Mkuu wa Tanzania alifikia hatua ya kuwapiga marufuku Wanasiasa kuingilia maamuzi ya Mahakama kwakuwa aliona muelekeo wake sio mzuri,Hongera sana. Lakini pia nielekeze pongezi zangu kwa Spika Job Ndugai ambaye naye mara kadhaa amechukua hatua za kinidhamu kwa wale 'wanaokengeuka' sheria na taratibu zilizopo kwenye mhilimili wange anaouongoza

Kama nilivyosema hapo awali kuwa nina mengi sana ya kuzungumza kwenye makala hii lakini hitoshe kusema tu kwamba Wanasiasa msivyokuwa macho na Siasa zenu mtatupeleka pabaya, Watanzania tunahitaji maendeleo, Watanzania tunahitaji Siasa kama daraja la kuelekea kwenye maendeleo na hatuhitaji kuiishi Siasa.
Tafakari, Tukutane makala ijayo.
0654920533/0746688032/0628599961

Post a Comment

 
Top