0
Football playersHaki miliki ya pichaSPORTPESA
Image captionSportPesa hudhamini klabu kadha zinazocheza Ligi Kuu ya Kenya
Kampuni ya mchezo wa kamari nchini Kenya, SportPesa, imesitisha udhamini wake wa michezo kutokana na uamuzi wa serikali kuongeza ushuru hadi asilimia 35 kutoka kwa asilimia 7.5.
Akizungumza na waandishi wa habari Jumanne, mkurugenzi mkuu na mwanzilishi wa SportPesa Ronald Karauri amesema wamelazimika kujiondoa kwa sababu hawawezi kudhamini michezo kama watatozwa ushuru wa asilimia 35.
Miongoni mwa michezo itakayoathiriwa na uamuzi wa SportPesa ni kandanda, ndondi na raga.
Kwa upande wa kandanda, kampuni hiyo hudhamini ligi kuu ya Kenya, timu za Gor Mahia, AFC Leopards na Nakuru All Stars pamoja na ligi ya Super 8.
"Sasa sisi tunaachia serikali mzigo huo wa kudhamini kandanda na michezo mingine. Kama wataweza ama hawataweza ni juu yao,'' anasema Karauri.

Pigo kubwa kwa soka Kenya

Kampuni hiyo ilipotangaza nia yake mwaka jana, afisa mkuu wa KPL Jack Oguda aliambia BBC kwamba hatua hiyo itakuwa pigo kubwa kwa soka Kenya.
Bw Karauri ameambia mwandishi wa BBC John Nene kwamba wamejaribu kila njia kuzungumza na wakuu wa serikali lakini hawakuelewana. Juhudi zao za mahakama kuingilia kati zimeambulia patupu.
"Mtu wa mwisho ambaye tunatarajia atatusaidia ni Rais Uhuru Kenyatta. Hivi sasa tunafanya mpamgo tukutane naye tumwelezee kwa undani kuhusu uamuzi wetu,'' anasema Karauri.
Licha ya uamuzi huo, Karauri amesema wataendelea kufanya kazi nchini Kenya, na kwamba hawataondoka.
Rais wa chama cha ndondi cha Kenya John Kameta amesikitishwa na uamuzi huo wa SportPesa lakini amelaumu serikali kwa kuongeza ushuru hadi asilimia 35.
Ronald Karauri
Image captionAfisa mkuu mtendaji wa SportPesa Ronald Karauri
"Hatuna budi ila kusimamisha ligi ya ndondi msimu huu kwa sababu sisi wenyewe hatutaweza kugharamia ligi yetu, ni pesa nyingi sana zinahitajika na kwa sasa hatuna mdhamini mwingine,'' amesema Kameta.
Miongoni mwa sababu za serikali kuongeza ushuru ni kupunguza idadi ya vijana wanaocheza kamari siku hizi.

Mazungumzo na serikali

Katibu mkuu wa wizara inayosimamia michezo nchini Kenya, Kirimi Kaberia, amesema Ijumaa hii wanakutana na kampuni zote za mchezo wa kamari ikiwemo SportPesa kujadili suala hilo la ushuru kuongezwa kwa asilimia 35 kutoka asilimia 7.5.
Kulingana na Kaberia mbali na kampuni za mchezo wa kamari, wahusika wengine watakaohudhuria mkutano huo ni maafisa wa mamlaka ya ushuru na wakuu wa michezo nchini Kenya hasa wale ambao wameathiriwa na uamuzi wa SportPesa kusitisha udhamini wao wa michezo nchini Kenya.
Hatahivyo Kaberia hakusema kwa undani kama kuna uwezekano wa serikali kupunguza kiwango cha ushuru huo wa asilimia 35 ambao serikali imeamua kutoza kampuni za mchezo wa kamari nchini Kenya..
Udhamini wa SportPesa kwa klabu za nje ya Kenya hautaathirika.
Kampuni hiyo kwa sasa hudhamini klabu za Uingereza, Everton an Hull City.
Mwaka jana Sportpesa waliingia Tanzania na kuanza kudhamini Simba inayocheza ligi kuu Tanzania na pia timu ya taifa ya Serengeti Boys.
SportPesa ni moja ya kampuni kubwa zaidi za mashindano ya kubashiri matokeo ya mechi Afrika Mashariki.

Uraibu wa kucheza kamari

Kodi hiyo ya juu iliidhinishwa na serikali kama moja ya njia za kuzuia watoto na vijana wa umri mdogo kujihusisha na mashindano hayo ya ubashiri wa matokeo.
Wakenya waliorodheshwa kuwa miongoni mwa watu wanaoshiriki sana katika mashindano ya bahati nasibu Afrika kusini mwa jangwa la Sahara na utafiti uliofanywa karibuni.
Utafiti huo ulionesha theluthi mbili ya Wakenya wa kati ya miaka 17 na 35 wamewahi kushiriki.
Wengi hutumia simu zao za rununu kubashiri matokeo ya ligi za nyumbani na ligi za nje, sana Ulaya.
Kumekuwepo na wasiwasi kuhusu athari ya uraibu huo kwa vijana. Wazazi na viongozi wa kidini walikuwa wameiomba serikali kuchukua hatua.
Bunge lilikuwa awali limependekeza kodi iwe 50%, lakini rais akapendekeza kodi hiyo ipunguzwe na mwishowe ikafikia 35%.

Post a Comment

 
Top