0
Shule ya sekondari ya Lupalilo inakabiliwa na ukosefu wa nishati ya umeme kwa zaidi ya mwezi mmoja hivi sasa, baada ya Transfoma iliyokuwepo kuungua na kusababisha kukwama kwa shughuli mbalimbali shuleni hapo ikiwemo wanafunzi kushindwa kujisomea usiku pamoja na kuhatarisha usalama wa wanafunzi baada ya kukosekana kwa nishati hiyo hasa nyakati za usiku

Akizungumzia Hali hiyo makamu mkuu wa shule Mwalimu LUNANILO KILATU amesema ni zaidi ya mwezi mmoja sasa wamekosa nishati hiyo baada ya transfoma kuungua na kupelekea baadhi ya shughuli kukwama shuleni hapo ikiwemo wanafunzi kushindwa kujisomea nyakati za usiku hivyo shule kulazimika kutumia jenereta ambalo amedai linawaongezea gharama zaidi.

Amesema wamesharipoti suala hilo kwa shirika la umeme TANESCO wilaya ya Makete tangu lilipotokea lakini hadi sasa ufumbuzi haujapatikana ingawa anaimani kuwa wanashughulikia.Kwa upande wa baadhi ya wanafunzi shuleni hapo waliozungumza na mwandishi wetu wamesema wanakumbana na changamoto nyingi baada ya kukosekana nishati hiyo ikiwemo kushindwa kujisomea nyakati za usiku huku wakihofia juu ya usalama wao hususani wanafunzi wa kike

Hata hivyo Tumemtafuta Meneja wa Tanesco wilaya ya Makete Ndugu HENRIKO RENATUS kupata ufafanuzi ambapo amesema mpaka sasa wanasubiri Transfoma nyingine kwani wameshatuma maombi ya kuomba transfoma na pindi zitakapowasili wataipa kipaumbele shule hiyo kutokana na uhitaji

Ni zaidi ya mwezi sasa shule hiyo ikabiliwa na tatizo hilo la ukosefu wa umeme na kukwamisha mambo mengi pamoja na usalama wa wanafunzi kuwa mdogo na kupunguza uwezekano wa wanafunzi kujisomea nyakati za usiku kama ilivyokuwa awali.Habari/picha na Edwin Moshi.


Makamu Mkuu wa shule akizungumza na mwandishi wetu ofisini kwake

Mwanafunzi wa Lupalilo Sekondari akizungumza na mwandishi wetu
Muonekano wa shule ya Lupalilo Sekondari

Transfoma iliyopata tatizo
 

Post a Comment

 
Top