0

Anti-government protester in EthiopiaHaki miliki ya pichaAFP
Image captionMaelfu wamezuiliwa tangu maandamano ya kuipinga serikali yalipoanza kfanyika
Ethiopian Prime Minister Hailemariam Desalegn looks on as he attends the opening ceremony for The Africa EU Summit in Abidjan on November 29, 2017Haki miliki ya pichaAFP
Image captionHailemariam Desalegn amesema kituo kipya cha kuwazuilia wafungwa kitafunguliwa
Waziri Mkuu wa Ethiopia ametangaza kuwa wafungwa wote wa kisiasa ambao wamekuwa wakizuiliwa korokoroni nchini humo wataachiliwa huru.
Aidha, amesema kituo hatari cha kuwazuilia wafungwa wa kisiasa ambacho kimekuwa kikitumiwa kuwatesa watuhumiwa pia kitafungwa.
Hailemariam Desalegn amesema kwenye kikao na wanahabari kwamba mashtaka yote dhidi ya wale ambao kesi zao bado hazijamalizika yatafutiliwa mbali.
Hatua hiyo, amesema, inalenga kutoa fursa ya kuwepo kwa mashauriano ya kisiasa.
Ethiopia kwa muda mrefu imetuhumiwa na makundi ya kutetea haki za kibinadamu kwa kuwakamata wapinzani wake kwa wingi na kuwazuilia katika juhudi za kuzima upinzani dhidi ya serikali.
Hata hivyo, hii ndiyo mara ya kwanza kwa serikali kukiri kwamba inawazuilia wafungwa wa kisiasa.
Mwandishi wa BBC Emmanuel Igunza anasema awali serikali imekuwa ikiwaita "wahalifu".
Shirika la kutetea haki za kibinadamu la Human Rights Watch (HRW) limekuwa likiituhumu serikali kwa kutumia sheria za kukabiliana na ugaidi kuwafunga wapinzani wake.
Shirika la Amnesty International limesema hatua ya leo huenda ikaachilia sura mpya kwa haki za kibinadamu Ethiopia.
Wafungwa hawa ni akina nani?
Wanaozuiliwa katika magereza na vituo mbalimbali kote nchini humo ni pamoja na wanaharakati wa upinzani kutoka majimbo ya Amhara na Oromia.
Majimbo hayo yalishuhudia maandamano ya kupinga serikali 2015 na 2016.
Kuna piawatu kutoka jimbo la watu wa mataifa ya kusini, na wanahabari ambao wamekuwa wakiikosoa serikali.
Ni vigumu kueleza hasa ni wafungwa wangapi wa kisiasa wanazuiliwa nchini humo, lakini mwandishi wetu anakadiria kwamba kuna takriban watu 1,000 wanaozuiliwa kwa makosa mbalimbali chini ya sheria za kupambana na ugaidi.
Anti-government protester in EthiopiaHaki miliki ya pichaAFP
Image captionMaelfu wamezuiliwa tangu maandamano ya kuipinga serikali yalipoanza kfanyika
Kuna wengine 5,000 ambao kesi zao bado zinasikizwa, wengi ambao walikamatwa wakati wa hali ya hatari Oktoba 2016.
Wataachiliwa kweli?
Serikali haijaeleza wataachiliwa lini au ni nani hasa wataachiliwa.
Kuna waliofungwa kwa sababu za kisiasa lakini kunao waliofungwa wakihusishwa na ugaidi.
Watu 19 waliohusishwa na kundi la Ginbot 7 linalochukuliwa na serikali kuwa kundi la kigaidi walifungwa jela wiki hii.

Nini hatima ya kituo kikuu cha kuwazuilia wafungwa?

Bw Hailemariam amesema kituo kikuu cha kuwazuilia wafungwa cha Maekelawi mjini Addis Ababa ambacho HRW tangu 2013 walidai kimekuwa kikitumia mateso kupata habari kutoka kwa washukiwa kitafungwa.
Serikali imesema kitageuzwa na kuwa makumbusho ya kisasa.
Kituo kipya cha kuwazuilia washukiwa kitafunguliwa na Bw Hailemariam amesema kitatimiza viwango vya kimataifa.

Post a Comment

 
Top