0
Wafuasi wa chama cha CCM wakati wa uchaguzi wa marudio Zanzibar mwaka jana 21 Machi baada ya Ali Mohamed Shein kutangazwa mshindiHaki miliki ya pichaAFP/GETTY
Shughuli ya kusukwa upya kwa safu ya uongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania itahitimishwa wiki hii katika mkutano mkuu unaofanyika mjini Dodoma, katikati mwa nchi hiyo.
Huu ni uchaguzi wa kwanza tangu Rais John Magufuli aliporithi uenyekiti kutoka kwa mtangulizi wake, Jakaya Kikwete.
CCM inaendeleza mikakati ya kurejesha hadhi yake baada ya ushindi uchaguzi wa mwaka 2015.
Licha ya kushinda urais kwa taabu, wapinzani chini ya mwamvuli wa UKAWA walipata karibu theluthi moja ya viti vyote vya ubunge na kudhibiti halmashauri katika miji muhimu ikiwemo Dar es Salaam, hii ikiwa ni rekodi mpya.
Miaka miwili ndani ya utawala wa Rais Magufuli, upepo unaonekana kugeuka.
Upinzani unaelekea kudhoofika, wakati CCM ikiimarika na kung'ara miongoni vyama vya ukombozi vilivyoleta uhuru katika nchi zao.
Ingawa haikuwepo wakati wa uhuru wa Tanganyika mwaka 1961 wala mapinduzi ya Zanzibar 1964, CCM inahesabika kama chama cha ukombozi kwa sababu kilizaliwa na vyama viwili vyenye sifa hiyo, TANU ya Tanganyika na ASP ya Zanzibar chini ya waasisi Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Abeid Amani Karume.
Wakati CCM ikizidi kuimarika, vyama vingi vilivyoanzishwa katika miaka ya 1950 na 60 vilishatimuliwa madarakani, vikiwemo United National Independence Party (UNIP), Malawi Congress Party (MCP) na Kenya African National Union, (KANU).
UNIP ya Kenneth Kaunda ilikuwa ya kwanza kuangushwa mwaka 1991 baada ya miaka 27 madarakani, ikafuatiwa na MCP ya Kamuzu Banda mwaka 1994 (miaka 29 madarakani) na kisha mwaka 2002 ikawa zamu ya KANU (miaka 39 madarakani).
Baadhi ya vyama vya ukombozi kama Parmehutu cha Rwanda, Mouvement National Congolais (MNC) cha Kongo- Kinshasa vilishafutwa miaka mingi.

Nini siri ya nguvu ya CCM?

Siri ya kwanza ya nguvu ya CCM ni Nyerere, Rais wa kwanza ambaye Watanzania wanamkumbuka kwa mapenzi makubwa wakimuita 'Mwalimu, au 'Baba wa Taifa.' Anaweza kuwa hakufanikiwa sana katika nyanja ya uchumi, lakini Nyerere alijenga taifa na kuwaunganisha Watanzania.
Pia, Nyerere alijijengea heshima kwa kung'atuka mwenyewe madarakani akiwa bado ana nguvu na kusimamia mchakato wa kumpata mrithi wake, kinyume na wengine waliosubiri watolewe.
Nchi chache zina watu wa hadhi ya Nyerere na Nelson Mandela wa Afrika ya Kusini.
Dkt Magufuli akiongoza mkutano wa Halimashauri kuu ya chama cha mapinduzi (NEC), Makao makuu ya CCM Dodoma JumapiliHaki miliki ya pichaIKULU, TANZANIA
Image captionDkt Magufuli akiongoza mkutano wa Halimashauri kuu ya chama cha mapinduzi (NEC), Makao makuu ya CCM Dodoma Jumapili
Hakuna kati ya Jomo Kenyatta wa Kenya, Dkt Hastings Kamuzu Banda wa Malawi wala Kenneth Kaunda, aliyewahi hata kupokonywa uraia wa Zambia, anayeheshimiwa katika nchi zao kama anavyoheshimiwa Nyerere.
Kutokana na mapenzi ya Watanzania kwa Nyerere na CCM yake, haikushangaza kwamba, mwaka 1991, matokeo ya Tume ya Rais iliyopewa jukumu la kukusanya maoni ya Watanzania juu ya mfumo wa vyama yalionesha kuwa asilimia 80 ya Watanzania walitaka chama kimoja kiendelee.
Bahati nzuri, mwenyewe aliunga mkono mfumo wa vyama vingi na sauti yake ikawa kura ya turufu.
Hata hivyo, wananchi wengi hadi sasa wanaiona CCM kama urithi wa Mwalimu hivyo kuasi chama hicho ni usaliti wa kumbukumbu yake.
Hii inaonesha kuwa vyama vingi si mtindo wa maisha ya kisiasa uliochaguliwa na Watanzania, bali ulianzishwa kwa sababu ilikuwa 'fasheni' ya wakati ule katika siasa mpya za dunia baada ya kudondoka kambi ya Mashariki ya Wajamaa.
Katika hali hii, uzoefu wa miaka 25 wa siasa za vyama vingi unaonesha kuwa Watanzania wanavitumia vyama vya upinzani kama mahali pa kuonesha hasira zao pale serikali ya CCM inaposhindwa kukidhi matarajio yao katika kusimamia uchumi na kupambana na ufisadi.
Kwa lugha za mtaani, CCM ni mke, upinzani ni kimada.
Wimbi la hivi karibuni la viongozi wa upinzani kuhamia au kurudi CCM na kudai kuwa hakuna haja ya upinzani kwa sababu ya mafanikio ya Rais Magufuli inathibitisha nadharia hii.

Demokrasia ndani ya chama

CCM ukilinganisha na kizazi cha vyama vyenzake vya ukombozi vilivyotimuliwa madarakani imekuwa ina demokrasia pana ya ndani ya chama na mifumo madhubuti ya kutatua migogoro na hivyo kukiwezesha kuhimili misukosuko.
Baada ya Nyerere kung'atuka, kumekuwa na kupokezana madaraka kwa marais watano mpaka sasa.
Kadhalika CCM imeweza kuvuka salama nyakati ngumu ikiwemo madai ya Serikali ya Tanganyika yaliyoibuliwa na wabunge 55 mwaka 1993 na shinikizo la wajumbe wa vikao vya halmashauri kuu na mkutano mkuu uchaguzi mkuu uliopita (2015) waliotaka Edward Lowassa awe mgombea urais wa chama hicho.
Ukiangalia vyama vya ukombozi katika nchi nyingine, vingi viliponzwa na ukosefu wa demokrasia na uwezo mdogo wa kushughulikia migogoro ya ndani.
KANU iliponzwa na Rais Daniel arap Moi aliyejaribu kuwachagulia Wakenya mrithi.
Naye, Dkt Banda wa Malawi alishajikabidhi uenyekiti wa chama na urais wa maisha wa nchi yake.
Wawili hawa walipalilia uasi ndani ya vyama vyao.
Huenda kiongozi mpya wa ANC, atakayemrithi Jacob Zuma atahitaji somo kutoka CCM kuepusha chama chake na zahma iliyovikumba vyama hivi.
ANC, kama CCM inajivunia muasisi, Nelson Mandela na uimara wa kitaasisi, lakini inahitaji Magufuli wake wa kufungua ukurasa mpya kwa ajili ya Afrika ya Kusini.

Mustakabali wa CCM mpya

Baada ya kupitia kipindi kigumu cha kushuka umaarufu wake hususan katika awamu ya pili ya uongozi wa Rais Kikwete, CCM inaelekea kurejesha hadhi yake, ikisaidiwa na faida ya mifumo imara wa uendeshaji wa chama, demokrasia ya ndani na historia iliyotukuka inayofungamanishwa na umaarufu wa muasisi wake.
Dkt Magufuli akisaliamiana na Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana akiwasili kuongoza kikao cha Kamati Kuu ya CCM mkoani Dodoma Disemba 15, 2017.Haki miliki ya pichaIKULU, TANZANIA
Image captionDkt Magufuli akisaliamiana na Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana akiwasili kuongoza kikao cha Kamati Kuu ya CCM mkoani Dodoma Disemba 15, 2017.
Hata hivyo, kwa upande mwingine, hadhi ya CCM inarejea kwa gharama kubwa kwa demokrasia changa ya Tanzania. Katika siku za hivi karibuni madiwani na wabunge wa upinzani wamekuwa wakihama vyama vyao kwa madai kuwa Rais Magufuli anafanya kazi nzuri.
Hata hivyo, wapinzani wanadai rushwa imekuwa ikitumika kuwashawishi wahamie CCM.
Kama hiyo haitoshi, Rais Magufuli amekuja na maagizo mapya juu ya namna ya kufanya siasa.
Hakutakuwa tena na mikutano ya siasa ya hadhara mpaka wakati wa uchaguzi isipokuwa kwa wabunge na madiwani katika maeneo yao.
Wakati huohuo, Rais Magufuli mwenyewe anafanya mikutano kama kawaida akichanganya shughuli za chama na serikali.
Kadhalika, viongozi wa upinzani wamejikuta matatani wakikamatwa na kushtakiwa kwa uchochezi pale wanapotoa matamshi mbalimbali, huku wengine wakihofia usalama wao baada ya kupokea vitisho.
Kwa ujumla tutegemee CCM mpya ya Magufuli kuimarika zaidi, lakini pia tutegemee kudorora kwa upinzani.
Si ajabu kwamba, baada ya miaka mitano ya Rais Magufuli, vyama vyaupinzani vitarejea katika hali yao ya miaka ya 1990 wakati wakipigania haki za msingi za kidemokrasia, badala ya kuzungumzia miradi ya maendeleo, mbadala wa ile ya CCM.
Bw Njonjo Mfaume ni mhadhiri msaidizi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

Post a Comment

 
Top