Nigeria wamepangwa kwenye kundi moja na Argentina kwa mara nyingine, Misri nao wakapangwa na Urusi na Uruguay baada ya droo ya Kombe la Dunia 2018 kufanywa nchini Urusi.
Panama, ambao wanacheza Kombe la Dunia mara ya kwanza wamepangwa na Ubelgiji na England na Tunisia.
Iceland, walioshangaza wengi kwa kufuzu, wamepangwa kucheza na Nigeria, Croatia na Argentina katika Kundi D.
Mechi ya ufunguzi itakuwa kati ya Urusi na Saudi Arabia.
- Mambo muhimu kuhusu nchi ambazo tayari zimefuzu Kombe la Dunia 2018
- Taifa la watu 335,000 lafuzu Kombe la Dunia
Droo kamili ya Kombe la Dunia:
- Kundi A: Urusi, Saudi Arabia, Misri, Uruguay
- Kundi B: Ureno, Uhispania, Morocco, Iran
- Kundi C: Ufaransa, Australia, Peru, Denmark
- Kundi D: Argentina, Croatia, Iceland, Nigeria
- Kundi E: Brazil, Uswizi, Costa Rica, Serbia
- Kundi F: Ujerumani , Mexico, Sweden, Korea Kusini
- Kundi G: Ubelgiji , Panama, Tunisia, England
- Kundi H: Poland, Senegal, Colombia, Japan.
Mpangilio wa mechi za makundi
Nani wanapigiwa upatu kushinda?
Mabingwa watetezu Ujerumani wanapigiwa upatu kushinda, wakifuatwa na Brazil, Uhispania, Argentina, Ufaransa, Ubelgiji na kisha England.
Ujerumani chini ya Joachim Low wanatafuta kuwa nchi ya kwanza kushinda Kombe la Dunia mtawalia tangu Brazil wakiwa na Pele 1958 na 1962.
Nani alivutia zaidi mechi za kufuzu?
Ujerumani hawajashindwa mechi hata moja ya fainali za au za kufuzu kwa Kombe la Dunia tangu nusu fainali ya 2010 dhidi ya Uhispania.
Walimaliza michuano ya kufuzu 2018 wakiwa wameshinda mechi 10 kati ya kumi walizocheza, na kufunga mabao 43. Walifungwa mara nne pekee.
Ubelgiji, Uhispania na England wote walimaliza mechi za kufuzu Ulaya bila kushindwa.
Brazil walitamba mechi za kufuzu Kombe la Dunia - lakini baada ya kumuondoa meneja Dunga na kumuingiza Tite.
Barani Asia, Iran walipitia makundi mawili bila kushindwa - mechi 18 bila kushindwa, ambapo mechi 12 kati ya hizo hawakufungwa bao hata moja.
Morocco walifuzu bila kufungwa bao hata moja katika kundi lao la kufuzu Afrika, ambapo walimaliza juu ya Ivory Coast.
Nani wanacheza mara ya kwanza?
Iceland ndiyo nchi ya kwanza pekee yenye raia ambao ni chini ya milioni moja kuwahi kufika Kombe la Dunia.
Hawakuwa wamefuzu kwa michuano mikubwa kabla ya kushiriki Euro 2016 ambapo waliwalaza England katika safari yao ya kufika robo fainali.
Panama, taifa la Amerika ya Kati, nao walifika Kombe la Dunia baada ya bao la ushindi la dakika ya 88 dhidi ya Costa Rica, bao ambalo pia liliwazuia Marekani kufuzu.
Nani miamba ambao wameachwa nje?
Walioshangaza zaidi walitoka Ulaya.
Mabingwa mara nne Italia walishindwa kufuzu kwa mara ya kwanza tangu 1958 baada ya kuondolewa na Sweden.
Uholanzi pia walishindwa kufuzu.
Jamhuri ya Czech, Wales, Scotland, Austria, Bosnia-Herzegovina na Uturuki ni miongoni mwa nchi nyingine za Ulaya zilizoshindwa kufuzu hatua ya makundi.
Jamhuri ya Ireland, Ireland Kaskazini na Ugiriki pia waliondolewa kwenye mechi za muondoano za kufuzu baada ya makundi.
Jimbo la Concacaf, Marekani walishindwa kufuzu kwa mara ya kwanza tangu 1986.
Barani Afrika, Ivory Coast, Cameroon na Ghana - wote ambao walishiriki Kombe la Dunia Brazil 2014 - pia hawakufuzu.
Chile, walioorodheshwa nafasi ya tisa duniani, pia walishindwa kufuzu.
Tiketi zinauzwaje?
Fifa wamepokea maombi 3.5 milioni ya tiketi, 300,000 yakiwa maombi ya tiketi za mechi ya fainali uwanjani Luzhniki.
Asilimia 57 ya maombi yametoka kwa wakazi wa je ya Urusi.
Tiketi ya bei nafuu zaidi ya fainali Kombe la Dunia ambayo raia asiye wa Urusi anaweza kununua ni ya £345.
Post a Comment