0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Mwenyekiti wa Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) Tabitha Siwale wakifunua kitambaa kuashiria ufunguzi wa maadhimisho ya miaka 10 ya chuo hicho Dar es Salaam jana. Kutoka (kwa waziri Mkuu) ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Prof Joyce Nadlichako, Mkuu wa ARU, Waziri Mkuu Mstaafu Cleopa Msuya, Makamu Mkuu wa ARU, Prof Evaristo Riwa na Rais wa Jumuiya ya ARU, Haruna Masebu. (Picha na Robert Okanda Blogs)

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (wa pili kushoto), Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Prof Joyce Nadlichako (wa nne kushoto), Mkuu wa ARU, Waziri Mkuu Mstaafu Cleopa Msuya (kushoto) na mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi wakionesha kitabu kilichozunduliwa wakati ufunguzi wa maadhimisho ya miaka 10 ya chuo hicho Dar es Salaam jana. Pamoja nao (wa tatu kushoto) ni Mwenyekiti wa ARU, Tabitha Siwale,  Makamu Mkuu wa ARU, Prof Evaristo Riwa (kulia) na Rais wa Jumuiya ya ARU, Haruna Masebu.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikata utepe kuashiria ufunguzi wa maadhimisho ya miaka 10 ya chuo hicho Dar es Salaam jana. Pamoja naye ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Prof Joyce Ndalichako (wa tatu kushoto), Mkuu wa ARU, Waziri Mkuu Mstaafu Cleopa Msuya (wa nne kushoto), mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi (wa tatu kulia), Mwenyekiti wa ARU, Tabitha Siwale (kushoto), Makamu Mkuu wa ARU, Prof Evaristo Riwa (kulia) na Rais wa Jumuiya ya ARU, Haruna Masebu.
Waziri wa Elimu, Sayansi naTeknolojia, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako
Mawaziri na Manaibu wa Wizara mbalimbali mliohudhuria ufunguzi huu,
Mkuu wa Chuo Mhe. Cleopa David Msuya,
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Mama Tabitha Siwale
Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Evaristo Liwa,
Manaibu Makamu wakuu wa Chuo,
Viongozi mbalimbali wa Serikali,
Vyama vya kitaaluma,
Wafanyakazi , Wanafunzi  na Wahitimu wa Chuo Kikuu Ardhi,
Wadau mbalimbali wa Elimu,
Waandishi wa Habari,
Mabibi na Mabwana;
Habari za asubuhi!
Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha sote kufika siku hii Muhimu ambapo tunashuhudia sherehe za kutimiza miaka kumi ya Chuo hiki toka kilipoanzishwa rasmi kuwa Chuo Kikuu kinachojitegemea hapo mwaka 2007. Hakika hii ni safari ndefu ambapo sasa ni muhimu kwa wadau wa Chuo hiki kuketi kwa pamoja na kujadili mustakabali wake katika kipindi kijacho.  
Aidha napenda kutoa pongezi kwa uongozi wa Chuo kwa kuona umuhimu wa kuandaa siku hii ambapo wadau mbalimbali wa Chuo wanakutana na kujadili maswala muhimu ya Chuo na yanayohusu ustawi wa jamii kwa ujumla. Hii ni fursa nzuri kwa wadau kuweza kutafakari kwa pamoja changamoto mbalimbali zinazo kabili chuo chetu na Taifa kwa ujumla na hatimae kuweza kupata ufumbuzi wa Changamoto hizo.  Hii ni miongoni mwa faida kubwa sana kwa mihadhara ya Wasomi kwani taifa letu kwa sasa linahitaji majibu zaidi ya changamoto zinazolikabili kuliko maswali.
Ndugu wanajumuia wa Chuo Kikuu Ardhi, huu sio wakati wa kujiuliza maswali tena bali ni wakati wa kutafuta suluhisho na ufumbuzi wa masuala mbalimbali yanayotuzunguka katika jamii yetu hasa katika sekta ya ardhi na maendeleo yake kama chachu ya kuleta tija katika uzalishaji.
Ndugu wanajumuiya ya Chuo Kikuu Ardhi
Mustakabali wa nchi yetu unaongozwa na Dira ya maendeleo ya Taifa, inayoweka mkazo katika kuifanya Tanzania kuwa nchi ya watu wenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025. Pamoja na mikakati mingine, taifa halina budi kuwa na wataalamu wa kutosha watakaohakikisha majukumu yote yanafanyika kwa umahiri na weledi. Hivyo Chuo Kikuu Ardhi kama taasisi ya Serikali yenye wajibu na mchango mkubwa katika kutayarisha wataalamu mbalimbali wa sekta za ujenzi, ukadiriaji majenzi na uhandisi wa mazingira, hakinabudi kutumia wataalam wake katika kutatua changamoto zinazo ikabili nchi kwa weledi na gharama nafuu.
Ninafahamu kuwa Chuo Kikuu Ardhi kimefanya tafiti mbalimbali katika jitihada za kubadili mfumo wa utendaji pamoja na kutatua changamoto zinazoikabili jamii yetu. Hili linafanyika wakati sahihi, kwa sababu kama mnavyofahamu mwelekeo wa Serikali yetu unalenga zaidi kupunguza gharama katika matumizi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miundombinu yake. Hivi karibuni Chuo kiliweza kuishawishi Serikali kutumia teknolojia mbadala ya ujenzi wa gharama nafuu, kwa ubora zaidi na kwa muda mfupi kupitia tafiti ya ujenzi iliyofanywa kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania na Baraza la Ujenzi la Taifa (NCC). Hii inatupa imani kubwa sisi upande wa Serikali na hivyo kuendelea kutambua mchango wa wataalamu wanaozalishwa na Chuo Kikuu Ardhi. Hivyo kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Chuo kilikabidhiwa shughuli ya ukarabati wa shule kongwe ishirini (20) za sekondari na vyuo vya mafunzo ya ualimu.
Ndugu Viongozi na wanazuoni wa Chuo Kikuu Ardhi
Tarehe 21 Septemba, 2016 nilipata nafasi ya kuhudhuria katika ufunguzi wa mradi wa Ujenzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha - Pwani, na nilikipongeza Chuo kwa kukamilisha ujenzi nadhifu wa Mahakama hiyo kwa Shilingi za Kitanzania million 520 ukilinganisha na wazabuni wengine walioomba kulipwa zaidi ya billion 1.7.  Binafsi mimi napata faraja nikiona hivi leo Chuo kinapoadhimisha miaka kumi tangu kuanzishwa kwa sababu nauona mwanga mwisho wa Taneli. Ni matumaini yangu kuwa juhudi nzuri zilizoanzishwa na Chuo, ambazo sasa zinaipa fursa Serikali ketembea kifua mbele katika masuala yote ya matumizi bora ya rasilimali ikiwemo rasilimali fedha zitaendelezwa na kupata maboresho ili kufikia lengo la Serikali.
Ndugu wadau wa Chuo Kikuu Ardhi
Aidha, napenda niutaarifu Umma huu kuwa hivi sasa Chuo Kikuu Ardhi ni miongoni mwa wataalamu washauri niliowateua kuishauri Serikali katika marejeo ya mpango kabambe kuendeleza mji wa Dodoma na kuhakikisha Serikali inahamia Dodoma kwa ufanisi. Ndugu zangu nafahamu pia hivi karibuni Chuo kiliongoza uandaaji wa mpango wa ujenzi wa shule mpya za sekondari na ukadiriaji wa gharama za majenzi kufuatia maafa ya tetemeko la ardhi yaliyoukumba mkoa wa Kagera. Shule hizo ni Kahoro na Nyakato. Hii ni baadhi tu kati ya michango mingi inayotolewa na Chuo Kikuu Ardhi.
Ndugu wadau wa Chuo Kikuu Ardhi
Mafanikio yote hayo niliyotaja hapo juu, bila shaka ni kutokana na kutoa mafunzo bora kwa fani mnazofundisha, hivyo ni wito wangu kwenu kuendelea kusimamia ubora wa elimu ili kuzalisha wataalamu watakaoenda kukidhi mahitaji mbalimbali ya soko kwenye jamii yetu. Nchi yetu bado inahitaji wataalamu wengi zaidi ili kuweza kupambana na changamoto mbalimbali hasa za miundombinu. Hivyo ni jukumu lenu kama taasisi ya Elimu ya juu kuzalisha wataalamu wengi zaidi bila kuathiri ubora wa Elimu.
Japokuwa ni kweli nimesikia kwenye hotuba ya Makamu Mkuu wa Chuo kuwa kuna changamoto mbalimbali zinazochangia ongezeko dogo la udahili kila mwaka na hivyo kukikosesha Chuo mapato ya ndani ya kutosha, bado Chuo kinapaswa kuongeza kasi ya tafiti zenye tija ili kutoathiri ubora wa elimu itolewayo Chuoni na kuhakikisha huduma nyingine zinapatikana. Kwa upande wa Serikali tunaamini kuwa matokeo ya tafiti mbalimbali ni chachu ya maendeleo ya taasisi za elimu ya juu kama tafiti hizo zitakuwa zimefikiriwa kwa mapana katika kuchangia kwa maendeleo ya Taasisi husika.
Ndugu Wadau wa Chuo Kikuu Ardhi
Napenda kusisitiza tena juu ya matumaini yangu kwa kusanyiko hili la leo kuwa tumieni fursa hii kujitafakari kuona mnaweza kuwekeza zaidi katika maeneo gani ili kuongeza tija ya uwepo wa Taasisi hii kwa jamii na Taifa. Wekeni mikakati madhubuti itakayowezesha Chuo kupiga hatua kubwa zaidi katika kipindi cha miaka Kumi ijayo. Siku zote mjikite kuwa bora zaidi ya wakati uliopita.  Fanyeni tafiti zenye kuleta majibu ya maswali na changamoto mbalimbali zinazolikabili taifa letu na Dunia kwa jumla. Kwa sasa, Tanzania inakabiliwa na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi, makazi, uharibifu wa mazingira, ujenzi holela, majanga ya asili kama vile mafuriko, matetemeko ya ardhi na mengineyo. Ninyi mkawe majibu ya changamoto zote hizo kwa kuwa na mchango wa kitaalamu wa kutatua changamoto hizo.
Kwa hotuba yangu hii fupi, natangaza rasmi kufungua sherehe hizi za ufunguzi wa Miaka Kumi ya Chuo KikuuArdhi.
Asanteni kwa kunisikiliza na nawatakia kila la heri!

Post a Comment

 
Top