0

Ligi kuu ya soka nchini England inaendelea leo kwa jumla ya michezo minne kuchezwa huku mchezo unaowavutia wengi zaidi ni ule kati ya wenyeji Watford watakaowakaribisha Manchester United.

Mchezo huo unatazamiwa kuwa na mvuto wa aina yake kutokana na kuwakutanisha makocha wawili kutoka nchini Ureno ambao ni Marco Silva wa Watford pamoja na Jose Mourinho wa Man United.

Manchester United inaingia kwenye mchezo wa leo ikiwa imetoka kupata ushindi wa pili mfululizo kwa kuifunga Brighton & Hove Albion FC bao 1-0, jumamosi iliyopita. Hata hivyo Man United itaingia kwenye uwanja wa Vicarage Road ikiwa na tahadhari kubwa kutokana na kupata kipigo cha mabao 3-1 msimu uliopita.

Watford ambayo inashika nafasi ya 8 ikiwa na alama 21 imekuwa imara msimu huu ambapo mechi yake ya mwisho iliichapa Newcastle mabao 3-0 jumamosi iliyopita.

Manchester United inayoshika nafasi ya pili ikiwa na alama 29 itakuwa na kikosi chake kamili baada ya wachezaji wake waliokuwa majeruhi kurejea uwanjani. Nahodha Michael Carrick ataendelea kuwa nje ya uwanja kutokana na kusumbuliwa na tatizo la moyo.

Post a Comment

 
Top