Msimamizi wa Ujenzi wa Kituo cha Kupoza Umeme cha Kigamboni kilichopo jijini Dar es Salaam, Sylvester Sikare (kulia) akielezea maendeleo ya ukamilishaji wa kituo kwa Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (katikati) mara alipofanya ziara katika kituo hicho tarehe 27 Novemba, 2017.
Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wilaya ya Kigamboni, Mhandisi Richard Swai (kushoto mbele) akieleza jambo kwa Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kulia) katika ziara hiyo.
Moja ya transfoma zilizopo katika kituo cha kupoza umeme cha Kigamboni kilichopo jijini Dar es Salaam. KUSOMA ZAIDI BOFYA HAPA
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akisalimiana na baadhi ya watendaji mara baada ya kuwasili katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Filberto Sanga.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kulia) akisaini kitabu cha wageni, mara baada ya kuwasili katika Kata ya Mkamba wilayani Mkuranga mkoani Pwani kabla ya kuanza kuwahutubia wakazi wa Kata hiyo. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Filberto Sanga.
Sehemu ya wakazi wa Kata ya Mkamba wilayani Mkuranga mkoani Pwani wakifuatilia hotuba iliyokuwa inatolewa na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (hayupo pichani).
Mbunge wa Mkuranga na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdalah Ulega akifafanua jambo kwa wakazi wa Kata ya Mkamba wilayani Mkuranga mkoani Pwani (hawapo pichani) katika mkutano wa hadhara.
Mkazi wa Kata ya Mkamba wilayani Mkuranga mkoani Pwani, Mohamed Masinike akiwasilisha kero yake kwa Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (hayupo pichani) katika mkutano wa hadhara.
******************************************
Na Greyson Mwase, Dar
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amesema kuwa kata za Kigamboni, Vijibweni, Tungi zinatarajiwa kupata umeme wa uhakika kufuatia kukamilika kwa mradi wa upanuzi wa kituo cha kupoza umeme cha Kigamboni kilichopo jijini Dar es Salaam.
Waziri Mgalu aliyasema hayo tarehe 27 Novemba, 2017 kwenye ziara yake katika kituo cha kupoza umeme Kigamboni na katika mikutano ya hadhara aliyoifanya katika kata za Kisiju na Mkamba zilizopo wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.
Alisema kituo hicho kitakuwa na uwezo wa kuhudumia wateja kutoka 6,000 hadi 12,000 na kuongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Nishati itahakikisha vituo vingine vya kuboresha hali ya umeme ndani ya jiji la Dar es Salaam vinakamilika mapema Desemba 15, 2017 na kuondoa tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara lililokuwa linajitokeza.
Aidha, alilitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kukamilisha vituo vingine vilivyobaki vya Kurasini, Gongo la Mboto na Mbagala mapema ili wakazi wa jiji la Dar es Salaam waweze kuondokana na tatizo la ukosefu wa umeme.
Katika hatua nyingine, Mgalu aliwataka wandarasi waliopewa kazi ya kujenga miundombinu ya kusambaza umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kukamilisha miradi mapema na kuongeza kuwa Serikali haitamvumilia mkandarasi atakayezembea ukamilishwaji wa mradi wake.
“ Wananchi wanahitaji umeme wa uhakika na kwa gharama nafuu, umeme ndio uchumi wa nchi na kama Wizara ya Nishati tupo kwa ajili ya kuhakikisha uchumi wa viwanda unakua kwa kuhakikisha nishati ya umeme ya uhakika inapatikana sehemu zote hasa vijijini,” alisisitiza Mgalu
Vilevile, Mgalu aliitaka REA kuainisha vipaumbele katika usambazaji wa umeme vijijini, kipaumbele kikiwa ni vijiji vyenye wakazi wengi na taasisi kama hospitali, makanisa na misikiti.
Akizungumzia suala la fidia kwa wakazi wanaopisha ujenzi wa miundombiniu ya umeme unaosimamiwa na REA, Naibu Waziri Mgalu alisema hakuna fidia kwa kuwa serikali imekwishagharamia gharama zote na kinachohitajika kwa wananchi ni kulipia gharama za Kodi (VAT) ambayo ni shilingi 27,000.
Aliwataka wakazi wa Kata za Kisiju na Mkamba wilayani Mkuranga kutandaza mifumo ya nyaya (wiring) kwenye nyumba zao au kununua kifaa maalum cha Umeme Tayari (UMETA) mapema kwa ajili ya kujiandaa na huduma ya umeme.
Akielezea mikakati ya Serikali katika kuhakikisha umeme unapatikana hususan katika wilaya ya Mkuranga yenye viwanda vingi, Naibu Waziri Mgalu alisema Serikali inatarajia kujenga kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia gesi Somanga Fungu na kusambaza gesi nyingine kwenye viwanda vitakavyohitaji.
Aliongeza kuwa Serikali inatarajia kuanza ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji wa Stieglers Gorge utakaokuwa na uwezo wa kuzalisha Megawati 2,100 na kukamilisha miradi ya Kinyerezi II na Kinyerezi III
Alisema kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2020 Megawati 5,000 zinapatikana na nchi kuingia kwenye uchumi wa viwanda utakaozalisha ajira kwa vijana hususan kwa vijana waishio vijijini.
“ Tunataka mazao yasindikwe vijijini na kusafirishwa ndani na nje ya nchi yakiwa kama bidhaa, tunataka mtumie fursa ya umeme kwa ajili ya uchumi wa viwanda badala ya matumizi ya majumbani tu,” alisema Mgalu.
Naye Mbunge wa Mkuranga ambaye ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdalah Ulega alimshukuru Naibu Waziri Mgalu kwa ziara yake katika wilaya ya Mkuranga na kuongeza kuwa wananchi wana matumaini makubwa ya umeme wa uhakika kwani wilaya hiyo imekuwa na changamoto ya ukosefu wa umeme kwa muda mrefu.
Post a Comment