Na. Ahmad Mmow.
WAKATI serikali ikiwa haiamini uchawi, na ikiwataka wanachi kutochukua sheria mkononi. Wananchi wanaoamini ushirikina na wanaojichukulia sheria mkononi wamechoma moto nyumba saba za makazi katika kijiji cha Nahukahuka A, wilaya na mkoa wa Lindi.
Baadhi ya mashuhuda walioshuhudia tukio hilo lilitokea jana alfajiri kijijini hapo, walisema sababu ya wananchi hao kuchoma moto ulioteketeza nyumba hizo saba za wananchi wenzao ni kutokanana kuamini kwamba mwenzao mmoja aliyepotea kijijini hapo katika mazingira ya kutatanisha siku tatu zilizopita na kuonekana ghafla juzi saa sita usiku alichukuliwa kichawi na wananchi waliowachomea moto nyumba zao.
"Kuna mtu alipotea katika mazingira ya kutatanisha siku tatu zilizopita, jana majira ya saa sita usiku alionekana akiwa katika hali mbaya nahajitambui. Wananchi wenye hasira kali walichukizwa na kitendo hicho, mapambazuko (alfajiri) wakachoma nyumba hizo moto, "alisema mmoja wa mashuhuda ambae hakutaka kutaja jina lake.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho Mussa Bakari Namwanga bila kutaja jina wala umri wa aliyepotea na kuonekana katika mazingira ya kutatanisha alikiri kuwa tukio hilo limetokea katika kijiji chake. Ambapo hadi alipozungumza na Muungwana kutoka katika kijiji hicho hakukuwa na mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo.
"Nikweli tukio hilo limetokea, wananchi wamechoma moto nyumba za wananchi wenzao kwa imani za kishirikina. Tukio hilo lilitokea alfajiri ya leo (jana) hivi navyozungumza nawewe, mheshimiwa diwani amekwenda Mtama kuripoti tukio hilo. Hakuna aliyejeruhiwa katika tukio hilo. Kwasasa bado hatujua kiasi cha mali ziliteketea na moto huo ," alisema Namwanga.
Maelezo ya mwenyekiti huyo juu ya mazingira ya tukio hilo na sababu za wananchi hao kufanya ukatili huo dhidi ya wananchi wenzao, hayakutofautiana na maelezo yaliyotolewa na shuhuda ambae alikataa jina lake liandikwe kwenye habari hii.
Kwa upande wake kamanda wa polisi wa mkoa wa Lindi, Renatha Mzinga alipoulizwa kuhusu tukio hilo, alisema hadi wakati huo alikuwa hana taarifa yoyote kuhusiana na tukio hilo. Huku akihaidi kufuatilia ili kupata ukweli.
"Mimi sina taarifa, ngoja nifuatilie kwawasaidizi wangu. Maana tumeamka kukiwa shwari, kwakifupi tumeamka kukiwa shwari, sasa kama kuna hilo acha nifuatilie, "alisema kamanda Mzinga.
Miongoni mwa vitendo ambavyo serikali imekuwa ikionya visivywe na wananchi ni kujichukulia sheria mkononi. Huku pia ikionya jamii kuacha imani za kishirikina. Ikiwamo ramli chonganishi.
Post a Comment