0
















WAKILI wa Utetezi, Joseph Makandege ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa mshitakiwa wa kwanza katika kesi ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha inayomkabili Herbinder Seth kuwa asipotibiwa ipasavyo, puto lililowekwa kwenye tumbo lake linaweza kupasuka na kusababisha kifo.

Makandege alidai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi na kueleza mahakama kuwa mshitakiwa huyo alifanyiwa upasuaji na kuwekwa puto tumboni.

Alidai kuwa  katika mashauri yaliyopita, mahakama ilitoa amri mara mbili, zote zikielekeza mshitakiwa huyo apelekwe Hospitali ya Muhimbili lakini haijatekelezwa.

Aliomba mahakama izingatie ugonjwa wa mshitakiwa na iamuru apelekwe moja kwa moja Muhimbili kwani  ndio hospitali ya juu  ya serikali nchini ambayo inategemea kuwa na wataalamu na vifaa stahiki vya ugonjwa unaomkabili.

"Upande wa jamhuri unatambua haya lakini kwa ridhaa yao wao wamempeleka mshitakiwa Amana hospitali. Swali ambalo mahakama isaidie kujibu pamoja na jamhuri, ni  je, kumpeleka mshitakiwa wa kwanza hospitali ya Amana,  magereza na jamhuri wameshindwa kutii amri ya mahakama?," alihoji Makandege.

“Mahakama haikumungunya maneno katika kutoa amri yake, ambapo ilitamka kwenye amri hiyo kwamba mshitakiwa huyo  apelekwe katika hosipitali ya taifa ya Muhimbili, wao kumpeleka Amana wametekeleza amri gani?” Makandege aliendelea kueleza.

Alidai  amri ya mahakama  haijatekelezwa hivyo upande wa mashitaka umekaidi amri hiyo.

"Mahakama ndio mahala amri zote zitaheshimiwa kwa pande zote mbili kwa kuwa nchi inafuata demokrasia na utawala wa sheria," alidai Makandege.

Makandege alidai kuwa kilichofanyika ni kinyume na amri ya mahakama na kinyume na sheria za magereza kifungu cha 53 (1) ambacho kinatoa fursa kwa mtu yoyote aliyeko gerezani kama anaumwa kufikishwa hospital ili apate matibabu.

Alidai kuwa ni rai yake kuwa mahakama haina uwezo wa kusikiliza shauri husika lakini inamamlaka ya kuhakikisha tararibu za mahakama zinafuatwa na kuhakikisha haki inatendeka.

Wakili wa Serikali, Vitalis Peter  alidai  hakuna amri yoyote ya mahakama ambayo jamhuri haijaitekeleza.

Alidai kuwa ni kweli kifungu cha 53 (1) cha sheria ya magereza kinaipa mamlaka magereza kumpeleka mtuhumiwa hospitali kama anaumwa na kwamba magereza wana wataalamu wao na hospitali yao na ndio wanakaa na mtuhumiwa na wanamuangalia kwa mara ya kwanza, wakishindwa kumtibu ndio wanampa rufaa.

Wakili Peter alidai kuwa mshitakiwa alihudumiwa na wataalamu wa magereza na kumpeleka hospitali ya juu yao  ambayo ni Amana, baada ya Amana alipatiwa matibabu na daktari bingwa kutoka muhimbili Dk Wilson Mgamba ambaye alimuona mtuhumiwa na kujiridhisha na afya yake.

"Wakili awasiliane na mteja wake kwanza kwasababu kashapatiwa matibabu na magereza hawachaguliwi kumpeleka mtu hospitali ambao ndio wanaweza kujua ugonjwa alionao na wapi pa kumpeleka," alidai Vitalis.

Baada ya kuwasilisha hayo, Wakili Makagande alidai kuwa haiwezekani daktari kuchukua vifaa vyote kuvipeleka katika magereza ya Segerea na kwamba mteja wake hajapatiwa matibabu hayo na yuko mahakamani anaweza kuongea mwenyewe.

Wakili Makandege alieleza mahakama kwamba kauli ya wakili wa serikali kudai kwamba Magereza hawapangiwi sehemu ya kumpeleka mtuhumiwa au mfungwa ambaye yupo mikononi mwao kwa matibabu, ni dharau kwa amri na heshima ya mahakama.

Pia aliongeza kuwa taratibu za ndani zilizowekwa na Magereza haiwezi ikawa juu ya amri za mahakama na sheria za nchi. “Uwepo kwa taratibu za magereza haiwezi ikaifanya amri za mahakama kusiginwa. Taratibu za ndani za magereza haiwezi ikawa juu ya amri za mahakama. Kauli hiyo ya wakili msomi mwandamizi wa serikali inaonyesha ni jinsi gani magereza wameidharau mahakama yako tukufu,” aliongeza Makandege.      

Hata hivyo, Hakimu Shaidi alisisitiza mshitakiwa huyo apelekwe katika hospitali ya Muhimbili kama ilivyotoa maagizo awali.

Kwa upande wake, James Rugemarila  aliiomba mahakama, magereza waweze kumruhusu kuonana na mawakili wake kwasababu anambambo mengi ya kuongea nao.

Alidai kuwa anamawakili 10 na kunawakati anahitaji kuongea nao lakini anauwezo wa kuwaona wawili tu hivyo anaomba aweze kupatiwa dakika 30 kuzungumza nao kabla hajarudishwa mahabusu.

Seth  na Rugemarila wanakabiliwa na mashtaka  12 ya  uhujumu uchumi  kwa kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu , kighushi,  kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu,  kutakatisha fedha  na kuisababisha hasara ya USD 22, 198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.

Post a Comment

 
Top