0
Police are seen on a street following an attack by gunmen on a restaurant in Ouagadougou, Burkina FasoHaki miliki ya pichaREUTERS
Image captionPolisi wakiwa na gari lisilopenya risasi walifika eneo hilo kukabiliana na washambuliaji
Watu 17 wameuawa na wengine wanane kujeruhiwa katika shambulio la kigaidi lililotekelezwa katikati ya mji mkuu wa Burkina Faso, Ouagadougou, serikali ya nchi hiyo imesema.
Watu walioshuhudia wamenukuliwa wakisema kwamba watu watatu waliokuwa na bunduki waliwafyatulia risasi wateja waliokuwa nje ya hoteli moja na mgahawa.
Eneo la katikati mwa jiji limezingirwa na maafisa wa jeshi na ubalozi wa Marekani mjini Ouagadougou umewatahadharisha raia wake wasiende eneo hilo.
Watu 30 waliuawa katika shambulio la kijihadi katika mgahawa mdogo ulio karibu na hapo Januari mwaka jana.
Kuna wasiwasi kwamba shambulio hilo huenda limetekelezwa na moja ya washirika wa mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda ambao bado wanaendesha shughuli zao katika eneo la Sahel, mwandishi wa BBC Alex Duval Smith amesema.
Waziri wa mawasiliano wa Burkina Faso Remis Dandjinou amesema haijabainika ni washambuliaji wangapi hasa waliohusika.
"Wamejibanza katika sehemu moja ya jumba waliloshambulia. Maafisa wa usalama wanaendesha oparesheni ya kuwafurusha," amesema kwenye televisheni.
Ufyatuaji wa risasi ulianza muda mfupi baada ya 21:00 (21:00 GMT) siku ya Jumapili katika barabara yenye shughuli nyingi ya Kwame Nkrumah.
Maeneo mawili, Hotel Bravia na Aziz Istanbul Restaurant, yanaonekana kulengwa na washambuliaji.
"Shambulio lilisababisha vifo vya watu 17, ambao uraia wake bado haujathibitishwa, na wanane wamejeruhiwa," taarifa ya serikali iliyonukuliwa na shirika la habari la AFP inasema.
Ouagadougou, Burkina FasoHaki miliki ya pichaREUTERS
Image captionMmoja wa waliojeruhiwa akiwa ameketi chini
Hospitali moja mjini humo ilisema mmoja wa waliouawa ni raia wa Uturuki.
Shambulio hilo linakaribiana sana na shambulio lililotekelezwa Januari 2016 ambapo watu wenye silaha walishambulia hoteli ya Splendid Hotel na mgahawa wa karibu wa Cappucino, pia katika barabara ya Kwame Nkrumah Avenue.
Watu zaidi ya 170 walishikwa mateka na 30 wakauawa.
Al-Qaeda walikiri kuhusika.
Burkina Faso inapatikana katika eneo la Sahel, ambalo linajumuisha pia nchi ya Mali ambapo makundi ya Kiislamu yamekuwa yakitekeleza mashambulio tangu mwaka 2012.
Map of West Africa


Post a Comment

 
Top