Mashabiki wengi wa ndondi wamelifutilia mbali pigano kati ya Floyd Mayweather na Muingereza Conor McGregor wakiitaja mechi hiyo kuwa 'kihoja' badala ya pigano.
Lakini maoni hayo ya kutoridhishwa na pigano hilo miongoni mwa mashabiki wa mchezo huo hayataathiri idadi ya watazamaji wake huku pigano hilo likitarajiwa kuonyesha katika runinga za zaidi ya mataifa 220 kuingana na naibu rais wa Showtime Stephen Espinoza.
Idadi hiyo ya watazamaji kutoke kote duniani inaweza kuipiku rekodi ya watazamaji ya watu milioni 4.6 iliowekwa wakati wa pigano kati ya Mayweather dhidi ya Manny Pacquiao 2015.
Watazamaji wa pigano hilo nchini Uingereza watalipa pauni 20 kila mmoja lakini wale wa Marekani watalipa pauni 75 kila mmoja.
Fedha hizi zikijumlishwa na mauzo ya tiketi ya kutazama pigano hilo ,ufadhili na biashara inaweza kuleta kiwango kikubwa cha fedha.
Tiketi pia zinauzwa kutazama pigano hilo katika vilabu katika mji wa Las Vegas, huku zaidi ya kumbi 400 za filamu pia zikilionyesha pigano hilo.
Hiyo inamaanisha kwamba takriban dola milion 600 zinaweza kupatikana, kiwango kinachokaribia kile cha pigano kati ya Mayweather na Pacquiao.
Mayweather anatarajiwa kujipatia dola milioni 300 huku McGregor akiweka kibindoni dola milioni 100.
Kumekuwa na ripoti kwamba Mayweather anaonekana kumpuuzilia mbali McGregor.
Wiki hii wachanganuzi watano wamesema kuwa hatua ya Mayweather kumpuuza mpinzani wake kunaweza kuwa hatari kubwa kwake.
Babake Mayweather Floyd jr, wiki hii alisema kuwa mwanawe amepoteza uwezo wake mkubwa tangu alipostaafu 2015.
Lakini iwapo atashinda pigano lake la hamsini katika maisha yake ataweza kuipita rekodi iliowekwa na Rocky Marciano ya kushinda mara 49 bila kushindwa.
Post a Comment