0
Kikosi cha idhaa ya BBC Pidgin
Image captionKikosi cha idhaa ya BBC Pidgin
Idhaa mpya ya utangazaji ya BBC, ambayo itakuwa ikipeperusha taarifa kupitia mtandao, imezinduliwa leo ambapo itatumia lugha ya Pidgin kutangazia wakazi wa Afrika Magharibi na Kati.
Pidgin ni moja ya lugha zinazozungumza zaidi katika kanda hiyo, ingawa haijatambuliwa rasmi.
Uzinduzi wa idhaa hiyo ni sehemu ya upanuzi mkubwa wa BBC World Service, kitengo cha shirika la BBC kinachohusika na utangazaji nje ya Uingereza, tangu miaka ya 1940.
Upanuzi huo unatokana na ufadhili wa serikali ya Uingereza ambao ulitangazwa 2016.
Pidgin itafuatwa hivi karibuni na idhaa 10 nyingine mpya katika bara la Afrika na bara Asia.
BBC World Service pia inapanga kuandaa makala zaidi za video na za kusomwa kwa kutumia rununu na pia kuangazia zaidi mitandao ya kijamii.
Kadhalika WS inapanga kuboresha matangazo yake ya runinga kore barani Afrika, ikiwa ni pamoja na kuanzisha zaidi ya vipindi 30 vipya vya runinga vya kupeperushwa na vituo washirika Afrika kusini mwa jangwa la Sahara.
Matangazo ya Idhaa ya Kiarabu na Idhaa ya Kirusi pia yataboreshwa chini ya mradi wa 2020.
Pidgin ni nini?
· Ni mchanganyiko wa lugha ya Kiingereza na lugha za asili ambao huwezesha watu wasiokuwa na lugha moja kuwasiliana.
· Kiingereza cha Pidgin Afrika Magharibi ilikuwa ndiyo lugha ya biashara iliyozungumzwa katika maeneo ya pwani wakati wa biashara ya utumwa katika bahari ya Atlantiki mwishoni mwa karne ya 17 na karne ya 18.
· Lugha hii hutumiwa sana Nigeria, Ghana, Cameroon na Equatorial Guinea
· Kimsingi ni lugha ya kutamkwa na kuzungumzwa, lakini hakuna aina ya kuandikwa ya lugha hii ambayo imeafikiwa.
'Kuvuka mipaka'
Ni vigumu kufahamu idadi hasa ya watu wanaozungumza lugha ya Pidgin, kwani huwa haifundishwi rasmi shuleni na pia wazungumzaji huifahamu kwa viwango tofauti.
Lakini nchini Nigeria, inakadiriwa kwamba watu kuanzia milioni tatu hadi milioni tano huitumia kama lugha yao ya kwanza katika shughuli zao za kila siku.
Inadaiwa kuwa lugha ya pili kwa watu karibu 75 milioni nchini Nigeria pekee, nusu ya raia wote.
Na pia huzungumzwa sana katika nchi nyingine katika kanda hiyo.
"Ni lugha ya biashara na mawasiliano isiyo rasmi. Ni lugha ambayo huwaunganisha watu na huvuka mipaka na vizuizi vyote - kikabila, kikanda na kijamii na kiuchumi," anasema
Bilkisu Labaran, mhariri anayeongoza idhaa hiyo mpya.
Ingawa kuna kituo cha redio kinachotumia Pidgin pekee, kituo cha Wazobia FM ambacho kilianzishwa miaka 10 iliyopita, BBC itakua ya kwanza kuanzisha tovuti na kuwa na mitandao ya kijamii.
Hili sana hutokana na kwamba si lugha iliyo rasmi, na hadi sasa hakuna aina iliyoafikiwa ya kuandika lugha hiyo.
" BBC itakuwa mwasisi katika hili," anasema Bi Labaran, mzungumzaji mzuri wa Pidgin.
Anatarajia changamoto - lakini pia kuna fursa kutokana na mjadala unaotarajiwa kuhusu kulainisha lugha hiyo, kuandikwa na kuzungumzwa kwake.
Kutakuwepo na nini?
BBC Pidgin itakuwa na mseto wa habari na makala za uchanganuzi wa kina zitakazoangazia matukio katika nchi ambazo lugha hiyo huzungumzwa na pia kimataifa - italeta ulimwengu kwa kanda hiyo, na kuiwasilisha kanda hiyo kwa ulimwengu.
Shirika hilo la utangazaji linasema idhaa hiyo ya dijitali pia itaangazia kuwavutia wasikilizaji na wasomaji wa umri mdogo pamoja na wanawake, ambapo mitandao ya kijamii itakuwa na mchango muhimu.
Kwa hivyo, hali kadhalika, kutakuwa na "Makala kuhusu utamaduni, burudani, ujasiriamali, sayansi na teknolojia, afya na michezo - ikiwa ni pamoja na Ligi Kuu ya England".
Kitovu cha idhaa hii kitakuwa Lagos, mji mkuu wa kibiashara wa Nigeria, lakini kutakuwepo na waandishi nchini Ghana na Cameroon pamoja na Nigeria kwenyewe, ambao watakuwa mashinani wakitafuta habari na makala.
Aidha, pamoja na Pidgin, raia wa Nigeria hivi karibuni watapokea idhaa nyingine mpya za Yoruba na Igbo , ambazo zitasaidia kuwafikia watu zaidi ya wanaofikiwa na Idhaa ya Kihausa na Kiingereza.
Idhaa hii mpya ya Pidgin itaanza kupeperusa rasmi taarifa na Makala kuanzia saa 0001GMT (saa kumi alfajiri Afrika Mashariki) siku ya Jumatatu 21 Agosti, na inapatikana katika anwani zifuatazo:
Pidgin - Umesema nini?
· I wan chop - I want to eat
· I no know - I do not know
· I no fit shout - I can't be bothered
· Wetin dey 'appen? - What is happening?
· How body? - How are you?
· Where you dey? - Where are you?

Post a Comment

 
Top