0
Picha inayohusiana
Chama cha *ACT Wazalendo* kimeshtushwa na kauli (amri) ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndugu John Pombe Magufuli aliyoitoa hivi karibuni akiwa Mkoani Tanga ya kutaka Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo ya Mazingara, Kata ya Mkata, Wilayani Handeni , katika Mkoa wa Tanga ahamishwe katika kituo hicho mara moja.

Hatua hiyo ni baada ya malalamiko ya mkuu wa wilaya ya Handeni , ndugu Godwin Gondwe kuwa kesi zote kati ya wakulima na wafugaji katika mahakama hiyo wanashinda wafugaji, na hivyo kumtuhumu hakimu huyo, aliyetajwa kwa jina moja la Laizer kuwa anapendelea wafuagaji.

*ACT Wazalendo* tunalaani kauli hii ya Rais kwa kuwa inakiuka misingi ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ibara 107B ambayo inaipa Mahakama Haki na Uhuru wa kufanya kazi yake bila kuingiliwa wala kubughudhiwa na mihimili mingine. Katiba inaainisha mgawanyo wa Madaraka baina ya Serikali, Mahakama na Bunge. 

Kitendo cha Ndugu Rais kutaka Hakimu wa Mahakama achukuliwe hatua kwa kuhamishwa ni kuuingilia Mhimili wa Mahakama ambao katiba na misingi ya utawala bora inahitaji mhimili huo pamoja na wanaohudumu wawe huru na kufanya kazi zao bila ya shinikizo la mtu yeyote iwe la kisiasa au kijamii.

Sisi *ACT Wazalendo* tunaamini kuwa hata kama tuhuma dhidi ya Hakimu mhusika ni za kweli, na kuwa ipo haja ya kuchukua hatua za kinidhamu dhidi yake, basi lazima utaratibu wa hatua hizo za kinidhamu kwa Hakimu huyo ufuatwe, kwa kuchunguzwa kwanza, kupata ushahidi na akikutwa na hatia basi achukuliwe hatua na mamlaka yake ya nidhamu, ambayo ni Tume ya utumishi wa Mahakama. Hatuamini kama hakimu anayedaiwa kupendelea katika kutoa hukumu anapaswa kuhamishwa tu.

Ni wazi kauli hii ya Rais inalenga kuwatia hofu Majaji na Mahakimu wengine. Na utekelezaji wake utaiaminisha jamii kuwa hatima za Majaji na Mahakimu katika kazi zao zipo mikononi mwa Rais na sio utaratibu wa Sheria uliowekwa. Amri hii ni batili, ni kinyume cha Katiba, na ikitekelezwa ni uvunjifu wa Katiba ya Nchi!

Katika jambo hili, *ACT Wazalendo* tunamtaka Kaimu Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma ajitokeze hadharani kukemea amri za namna hii zinazoudogosha mhimili wa mahakama, atoe kauli ya kuwahakikishia Mahakimu na Majaji kuwa usalama wa majukumu yao (security for tenure) unalindwa na utaendelea kulindwa kwa mujibu wa Sheria na Katiba ya Nchi. Na kuwa kama yapo malalmiko juu ya hakimu Laizer basi utaratibu ufuatwe.

*ACT Wazalendo* pia inamsihi Rais kumchukulia hatua za kiutawala Mkuu wa Wilaya ya Handeni Bwana Godwin Gondwe Kwa kumwingiza Rais kwenye mgogoro wa kikatiba usio wa lazima. Mkuu wa Wilaya ni mjumbe wa vikao vya ngazi za chini vya michakato ya kutazama maadili ya mahakimu na anajua taratibu za kufuata. Alichofanya Mkuu wa Wilaya ni kitendo kinachopaswa kukemewa kwa hatua kali kuchukuliwa dhidi yake ikiwemo kumwajibisha ili iwe fundisho kwa Wakuu wa Wilaya wengine wanaoshindwa kufanya kazi zao.

Mwisho, tunavitaka vyama vya mawakili vya Tanganyika na Zanzibar na taasisi nyengine zenye kupigania utawala wa Katiba na Sheria nchini kujitokeza na kulaani kauli ya Rais na kumshinikiza Rais au kupitia waziri wake wa Katiba kuwaomba radhi watanzania kwa jaribio hili la kutaka kuvunja misingi ya katiba waliyoapa kuilinda.

Thomas E. Msasa
Mwenyekiti- Kamati ya Sheria na Katiba
ACT Wazalendo 
Agosti 09, 2017

Post a Comment

 
Top