Na Bashir Yakub.
SHERIA ZILIZOPITIWA :
1. Sheria ya Mwenendo wa Kesi za Jinai, Sura ya 20.
2. Sheria ya Huduma za Mashtaka kwa Taifa, Na. 27/2008.
3. Kanuni za Adhabu, Sura ya 16.
_______________
Tundu Lissu anasema anaamua kumshitaki Makonda kwa kosa la kughushi nk. kwa kuwa Serikali imekataa na haioneshi nia ya kumfikisha mahakamani Makonda.
Kama sababu ni kuwa serikali imekataa kumpeleka Makonda mahakamani ndio maana Tundu Lissu na wenzake wanaamua sasa kuchukua hatua basi nao hawatafanikiwa.
Kwa sheria ilivyo hawatafanikiwa mpaka serikali wanayosema haitaki itake. Kwa mujibu wa kifungu cha 97 cha Sheria ya Mwenendo wa Kesi za Jinai kazi ya kufungua na kuendesha mashtaka yote ya jinai ni kazi ya serikali kupitia ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Jinai (DPP).
Hata hivyo kwa mujibu wa kifungu cha 99(1) cha sheria hiyohiyo ni kweli bila ubishi kuwa mtu binafsi au Wakili yeyote binafsi kama alivyo Tundu Lissu naye anaweza kufungua na kuendesha mashtaka ya jinai dhidi ya mtu yeyote mkosaji kama ilivyo kwa DPP wa serikali.
Pamoja na hayo kifungu cha 97 cha sheria hiyo ya Mwenendo wa Kesi za Jinai kinasema kuwa ikiwa mashtaka yamefunguliwa na mtu binafsi au Wakili binafsi kama alivyo Tundu Lissu basi mwendesha mashtaka wa serikali akiamua anaweza kuchukua kesi hiyo.
Pia kifungu kinasema zaidi kuwa Wakili huyo binafsi katika kesi hiyo aliyofungua atalazimika kufuata maelekezo ya mwendesha mashtaka huyo wa serikali wakati wote wa kesi.
Maana yake ni kuwa ikiwa mwendesha mashtaka wa serikali atamwamuru Tundu Lissu kubadili jambo lolote katika kesi aliyofungua basi atalazimika kulibadilisha. Lakini kubwa kuliko yote ikiwa mwendesha mashtaka wa serikali atamwamuru Tundu Lissu kufuta kabisa kesi ya Makonda basi atalazimika kuifuta. Hii ndio maana ya kifungu hicho.
KUSOMA ZAIDI sheriayakub.blogspot.com
Post a Comment