RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed
Shein amewataka mabalozi wanaokwenda kuiwakilisha Tanzania nchi za nje kuhamasisha wawekezaji kuja kuwekuza hapa nchini hasa katika sekta ya
viwanda.
Akizungumza na Mabalozi Wateule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
waliofika Ikulu kumuaga pamoja na kufanya nae mazungumzo, Rais Shein amesisitiza
kuwa sekta ya viwanda imepewa
kipaumbele na kutiliwa mkazo mkubwa na Serikali zote mbili.
Mabalozi hao ni pamoja na Balozi Emmanuel Nchimbi ambaye anakwenda
kuiwakilisha Tanzania nchini Brazil, Balozi Mbelwa Kairuki anaekwenda nchini
China, Balozi Geogre Kahema Madafa anaekwenda Italy, Balozi Profesa Elizabeth
Kiondo anakwenda nchini Turkey.
Wengine ni Balozi Dk. James Msekela UN nchini Geneva, Balozi Samwel
Shelukindo anaekwenda Paris, France na Balozi mteule Lt. Jeneral (Mstaafu) Paul
Mella anaekwenda D.R. Congo.
Dkt. Shein ameeleza haja ya Mabalozi hao kuitangaza Zanzibar na Tanzania
nzima kiutalii ambapo kwa upande wa Zanzibar sekta hiyo imekuwa ni muhimu
kutokana na kuchangia asilimia 80 ya pato la Taifa.
Ambapo amesisitiza haja ya kuvitangaza vivutio vya kitalii vilivyopo nchini
vikiwemo Mbuga za wanyama, sehemu za kihistoria, fukwe na vyenginevyo.
Nao Mabalozi hao walimthibitishia
Dk. Shein kuwa wamepokea maelekezo yote aliyowapa na kuahidi kuyafanyia
kazi hasa kwa maeneo maaluma ya Zanzibar na Tanzania Bara.
Post a Comment