0

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam imefanya upasuaji kwa njia ya matundu madogo kwa watoto tisa waliozaliwa na matatizo ikiwa ni utaalamu mpya nchini.

Upasuaji huo umefanyika katika kambi ya siku tatu iliyoanza Februari 20, mwaka huu. Hospitali hiyo imesema itaendelea kuboresha huduma za upasuaji kuendana na teknolojia.

Akizungumza baada ya kukamilisha upasuaji wa mwisho katika chumba cha upasuaji katika hospitali hiyo juzi, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto wa Hospitali ya Muhimbili, Zaituni Bokhary amesema wamefanikiwa kufanya salama na kwamba afya za watoto wote waliofanyiwa upasuaji zinaendelea vizuri.

“Aina hii ya upasuaji tumefanya kwa mara ya kwanza hapa kwetu na tumefanikiwa, upasuaji huu tumeshirikiana na wenzetu wa Hospitali ya King Faisal ya Saudi Arabia,” alisema Dk Bokhary na kuongeza kuwa upasuaji huo umefanyika kwa mafanikio makubwa na kwamba hakuna hitilafu yoyote iliyojitokeza.

“Upasuaji huu tuliofanya ulikuwa wa kushusha kokwa za korodani kwa mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka minane, kokwa hazikushuka kama ilivyotakiwa kufanyika katika hali ya kawaida ndio maana leo tumemfanyia upasuaji,” alifafanua daktari huyo.

Daktari huyo alisema mwaka jana walimfanyia upasuaji wa awali mtoto huyo ambapo walisogeza karibu kokwa zake kwani zilikuwa mbali tumboni, "leo tumezishusha kabisa kwenye korodani zake,” alieleza.

Akifafanua alisema kokwa za kiume zinatakiwa kushuka na kukaa katika vifuko vya korodani na si kubaki ndani kwani baadaye anapokuwa mtu mzima hushindwa kutungisha mimba.

Mbali na upasuaji wa mtoto huyu ambaye ameshushwa kokwa zake katika korodani, wengine wamefanyiwa upasuaji wa kutengenezewa njia ya haja kubwa, kutanua njia ya chakula ambayo mwanzo ilikuwa imebana na mwingine upasuaji wa kurudisha utumbo wake ndani kwani ulikuwa ukitoka nje kila alipokuwa akijisaidia.

Post a Comment

 
Top