Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kwa kauli moja limewaita mbele ya Kamati yake ya Haki, Maadili na
Madaraka ya Bunge Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, na DC wa
Arumeru Alexander Mnyeti kwa madai ya kudharau Bunge.
Maamuzi hayo ni sehemu ya maazimio manne ya Bunge yaliyopishwa usiku
huu dhidi ya viongozi wanaoteuliwa na Rais hasa wakuu wa mikoa na
wilaya, ambapo azimio lingine ni kumtaka Waziri wa TAMISEMI kutoa
maelekezo kwa wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kufanya kazi kwa mujibu
wa sheria na kutoingilia majukumu yasiyo yao.
Hatua hiyo inafuatia hoja iliyotolewa bungeni hapo na Mbunge wa Ukonga,
Mwita Waitara, kufuatia kauli inayodaiwa kutolewa na Mkuu wa Mkoa wa
Dar es Salaam Paul Makonda inayodaiwa kuwa ni dharau kwa Bunge.
Pia Mwita amedai kuwa viongozi mbalimbali hasa wakuu wa mikoa na wkuu wa
wilaya wamekuwa wakitumia madaraka yao vibaya kiasi cha kuingilia
majukumu yasiyo yao, na wakati mwingine kuingilia majukumu ya Bunge, na
kutolea mfano Paul Makonda na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha,
Alexander Mnyeti.
Baada ya hoja yake kukubaliwa na Mwenyekiti wa kikao hicho Mh Andrew
Chenge, wabunge wameijadili ambapo wabunge kadhaa akiwemo Ester Bulaya,
Zitto Kabwe, Saed Kubenea na Joseph Musukuma wamepata fursa ya kuchangia
ambapo kwa kiasi kikubwa wote wameoneshwa kukerwa na kauli hiyo
inayodaiwa kutolewa na Paul Makonda, pamoja na utaratibu wa wabunge
kukamatwa bila utaratibu.
Wakati mbunge Zitto Kabwe akipendekeza kuitwa mbele ya kamati viongozi
waliotuhumiwa, Ester Bulaya amepasua jipu kwa kusoma ujumbe wa vitisho
aliodai umetoka kwa kiongozi mmoja aliyeteuliwa na Rais.
Akichangia mjadala huo, Waziri anayehusika na Bunge pamoja na sera Mh.
Jenista Mhagama amewataka wabunge kutomuhusisha Rais Magufuli na makosa
yanayofanywa na viongozi aliowateua ambapo amesema kuwa kwa mujibu wa
sheria Rais ana majukumu yake, na wakuu wa mikoa na wilaya wana wajibu
wao, hivyo kama kuna RC au DC anakwenda kinyume na sheria au kuingilia
Bunge, anapaswa kuwajibishwa mwenye.
Baada ya mjadala huo, Chenge amewahoji wabunge wanaokubaliana na
mapendekezo ya mtoa hoja, ambapo wabunge wote wameitikia kuunga mkono
mapendekezo hayo manne na kuwa maazimio rasmi ya Bunge.
Post a Comment