0


RAIS wa  Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Zanzibar imepiga hatua kubwa katika mafanikio ya kimaendeleao
                    


Dk. Shein aliyasema hayo huko katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani, MnaziMmoja Mjini Zanzibar wakati akifungua Semina ya siku moja kwa Viongozi na Watendaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu Umuhimu wa Takwimu na Matumizi yake.

Katika maelezo yake, Dk. Shein alisema kuwa hakuna  sababu ya kuyabeza maendeleo makubwa yaliopatikana hapa nchini lakini kuna kila sababu ya kutatua changamoto ya kutokuwepo kwa takwimu sahihi katika taasisi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Dk. Shein ambaye pia, alikuwa Mwenyekiti wa Semina hiyo, alisema kuwa kutokana na hali hiyo ndio maana akaona haja ya kuandaliwa mafunzo hayo ambayo yatasaidia kwa kiasi kikubwa kufikia malengo yaliokusudiwa ambapo mwishoni yatakuja na maazimio ambayo hatimae yatafanyiwa kazi.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa hakuna jambo lolote la maendeleo linaloweza kufanyika na kufanikiwa bila ya kuwepo kwa takwimu sahihi na ufanyaji tafiti huku akisisitiza kuwa upatikanaji wa takwimu sahihi na kwa wakati ni msingi muhimu katika kupanga na kutekeleza mipango yote ya maendeleo.

Rais Shein alieleza kuwa juhudi mbali mbali zimechukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutatua changamoto hiyo ikiwa ni pamoja na kuunda Idara ya Sera na Utafiti, Sheria ya Takwimu lakini bado changamoto hizo zimekuwepo, hivyo aliwataka washiriki wa Semina hiyo kufuatilia kwa makini mafunzo hayo na kuyafanyia kazi ipasavyo.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alisema kuwa kwa upande wa Takwimu Zanzibar imekuwa ikifanya vizuri na kutumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.  

Pia, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee,Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana pamoja katika kuandaa  Semina hiyo.

Post a Comment

 
Top