0


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein  amesikitishwa uwepo wa baadhi ya Mawakili ambao  walioacha kusoma Katiba ya Zanzibar na kuifahamu vizuri na kuanza kuituhumu Mahkama kuwa inatumika kisiasa, au kuhoji nje ya utaratibu wa Mahkama maamuzi yanayotolewa na vyombo halali vya Kikatiba katika kusimamia utoaji haki.
                       


Dk. Shein aliyasema hayo leo katika Sherehe ya Siku ya Sheria Zanzibar, iliyofanyika huko katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani, huko Kikwajuni mjini  Zanzibar.

Katika hotuba yake kwa wananchi, Dk. Shein alisema kuwa tabia hiyo si katika maadili, mila, silka na desturi za Mawakili ambao taaluma yao imetukuka na ambao wanatakiwa kuisaidia Mahkama katika kutenda na kutoa haki.

Dk. Shein alisema kuwa jambo la kushangaza zaidi ni pale baadhi ya Mawakili hao kuvaa majoho yao ya kisheria asubuhi na kwenda kutetea wateja wao Mahkamani, ambao wamewatoza kiwango kikubwa cha fedha, wakitambua kuwa Mahkama ndio chombo pekee cha kikatiba cha kutoa haki lakini hugeuka na huvaa fulana za vyama vya siasa na kuaza kuishutumu Mahkama kuwa ni chombo kinachotumika kisiasa.

Alisema kuwa tabia hiyo inayofanywa na baadhi ya Mawakili hao ni kuingilia uhuru wa Mahkama katika kutimiza majukumu yake ya kikatiba ya utoaji wa haki.

“Naamini kwamba Mheshimiwa Jaji Mkuu, una uwezo wa kuwashughulikia Mawakili wa aina hii, wanaoitia dosari na kuleta taswira mbaya kwa jamii katika chombo hiki cha Mahkama unachokiongoza na ambacho Majaji wake wamepewa kinga ya Kikatiba katika kufanya kazi na kutimiza majukumu yao ya kutoa haki”,alisisitiza Dk. Shein.

katika hatua nyengine Dr Shein ametoa wito kwa Jaji Mkuu wa Zanzibar kuhakikisha kuwa pale anapotumia uwezo na mamlaka yake aliyopewa na Sheria ya Mawakili Sura ya 28, ya kusajili na kutoa vyeti vya kufanya kazi za Uwakili, anatumia uwezo na mamlaka hayo kwa kusajili Mawakili wenye maslahi ya kuitumikia jamii na sio wanaharakati wanaotumia vibaya taaluma yao.

Post a Comment

 
Top