WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakuu wa mikoa ya Singida, Mbeya, Iringa na
Dodoma wawasimamie wananchi wao na kuhakikisha hakuna shughuli za kibinadamu
zinazofanyika ndani ya vyanzo vya maji.
Ametoa
kauli hiyo leo alipozungumza na watumishi wa kituo cha kuzalisha umeme cha
Mtera alipotembelea bwawa la Mtera akiwa njiani kwenda mkoani Njombe kwa ziara
ya kikazi.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo baada ya Kaimu Meneja wa Kituo cha kuzalishia umeme cha
Mtera, Mhandisi Edmund Seif kutaja baadhi ya changamoto zinazokikabili kituo
hicho kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu ndani ya vyanzo
vya maji.
Kufuatia
hali hiyo Waziri Mkuu ameagiza kufanyika vikao vya ujirani mwema ili wananchi
waelimishwe umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji na ni marufuku
kuendesha shughuli za kibinadamu ndani ya kilomita 60 kutoka kwenye chanzo.
Awali, Mhandisi Seif
amesema kituo hicho cha Mtera kinazalisha megawati 80 kwa siku ambazo
zinaingizwa kwenye gridi ya Taifa ambapo amesisitiza kuwa bwawa hilo kwa sasa
lina maji ya kutosha kuzalisha umeme hadi msimu ujao wa mvua.
Post a Comment