WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amemwagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Kamishna
Msaidizi wa Polisi, Zuberi Mwombeji awakamate maafisa wanne na kuhakikisha
wanapelekwa Masasi chini ya ulinzi ili wajibu tuhuma za upotevu wa tani elfu
mbili mia moja na 38 za korosho.
Maafisa hao ni
Kaimu Meneja Mkuu Chama Kikuu cha Ushirika cha Masasi (MAMCU), Bw. Kelvin
Rajab na Meneja Tawi wa MAMCU, Bw. Lawrence Njozi.
Wengine ni wakurugenzi wa kampuni ya YURAP ya Masasi inayohusika na uhifadhi wa
mazao kwenye maghala, Bw. Yusuph Namkukula na Bw. Ramadhani Namakweto.
Waziri Mkuu
alifikia uamuzi huo kwenye kikao alichokiitisha Songea mjini baina
ya watendaji kutoka Bodi ya Korosho Tanzania, MAMCU, wamiliki wa ghala la BUCO
- Masasi na kikundi cha wakulima sita waliowawakilisha wenzao kutoka vyama vya
msingi (AMCOS) vya wilaya za Mtwara na Masasi.
Katika kikao
hicho, Waziri Mkuu alitaka apatiwe maelezo ya kina ni wapi zilipo hizo tani elfu
2 mia moja na 38 za korosho wakati taarifa waliyompatia viongozi hao jana
inaonyesha kuwa waliuza korosho zote na hakuna hata kilo moja ambayo
haijanunuliwa katika mnada wa tano uliofanyika Novemba 10, mwaka jana.
Kaimu Meneja
Mkuu wa MAMCU, Bw. Kelvin Rajab alikiri mbele ya Waziri Mkuu kwamba korosho zote
ziliuzwa na zilishalipwa na wanunuzi wa mnada wa tano lakini akadai hakupewa
taarifa ya kukosekana kwa kiasi hicho cha korosho.
Naye mmiliki wa
ghala la BUCO, Bw. Ramadhan Namakweto alikiri kupokelewa kwa korosho hizo
ghalani kwake lakini akashindwa kutoa maelezo ni kwa nini hazionekani zilipo.
Tuhuma
zinazowakabili maafisa hao wanne ni kuwalipa kilo pungufu ya zile zilizowasilishwa
ghalani, wakulima wa korosho katika wilaya ya Masasi na kutowapa maelezo yoyote
juu ya upungufu huo.
Kutokana na mapungufu hayo, Waziri Mkuu aliagiza
watu hao wapelekwe Masasi chini ya ulinzi ili uchunguzi ufanyike na pia amemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
afanye ukaguzi wa hesabu za MAMCU na kujiridhisha kiasi cha korosho
kilichonunuliwa; fedha zilizolipwa na kuingia akaunti za MAMCU; kiasi cha fedha
zilizolipwa kwa vyama vya msingi na wananchi kwa ulinganifu na bei ya korosho
kwa kila mnada husika.
Mapema, wakisoma
risala yao kwa Waziri Mkuu, wakulima hao walisema wana kero nyingi sana kama
vile kutolipwa fedha zao kwa wakati; kutoeleweka mahali zilipo korosho ambazo
walishaziuza kwa MAMCU, kukatwa makato ya unyaufu ambayo Serikali ilikwishapiga
marufuku na kutosikilizwa malalamiko yao na viongozi wa MAMCU pamoja na
viongozi wa mkoa na wilaya.
Wakulima hao wa korosho kutoka Masasi mkoani Mtwara
walikutana Januari 3, 2017 katika kijiji cha Chiungutwa na kuazimia kuwa wangeandamana
hadi Dar es Salaam ili wawasilishe kilio chao kwa Waziri Mkuu au kwa Mheshimiwa
Rais Dk. John Magufuli.
Kwa kutambua umbali uliopo kutoka Masasi hadi Dar es
Salaam na kwamba yeye hakuwepo katika siku waliyopanga kwenda huko, Waziri Mkuu
aliamua kuwaita wakulima hao wamfuate Songea ambako alikuwa na ziara ya kikazi
ya siku nne.
Post a Comment