0

WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) umechukua hatua za haraka, kwa kumuondoa kwenye nafasi yake Meneja wa Mkoa wa Simiyu, Michael Semfuko na kumrejesha Makao Makuu Dar es Salaam kupisha uchunguzi.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya Rais John Magufuli kukataa kukubaliana na gharama ya Sh bilioni 46 ya kujenga Hospitali ya Mkoa wa Simiyu.

Aidha, TBA imeunda kamati ya wataalamu kwenda Simiyu kuchunguza kujua uwiano wa mradi huo na gharama iliyoelezwa na meneja huyo kwa Rais akiwa kwenye ziara huko.

Rais Magufuli akiwa ziarani Simiyu wiki iliyopita, aliweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo, lakini hakukubaliana na gharama ya Sh bilioni 46 iliyotajwa ili kukamilisha mradi huo badala yake alitaka ijengwe kwa Sh bilioni 10.

Uamuzi wa kumng’oa meneja huyo wa mkoa, uliwekwa wazi Dar es Salaam jana na Mtendaji Mkuu wa TBA, Elius Mwakalinga wakati wa ziara ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Simiyu, kuzungumzia mradi huo pamoja na kutembelea miradi inayosimamiwa na TBA, ikiwa ni agizo alilopewa Mkuu wa Mkoa, Antony Mtaka na Rais.

“Kisheria miradi yote ya ujenzi kwenye mikoa yote huwa inasajiliwa TBA, lakini cha kushangaza mradi huu haukuwa umesajiliwa na sielewi, lakini sitaki kusemea tutakapofika huko tutajua ni kwa nini imekuwa hivyo,” alisema Mwakalinga.

Aliongeza kuwa meneja huyo atatakiwa kutoa maelezo, ikiwa ni utaratibu wa serikali aeleze kwa nini alifikia hatua ya kuzungumzia, mradi ambao haujasajiliwa.

“Inawezekana meneja alipewa mradi siku hiyo au alikuwa anaupitia ili aulete kwetu, yote hayo tutayajua baada ya maelezo yake,” alieleza mtendaji huyo.

Akizungumzia zaidi mradi huo wa Simiyu, alisema wameunda kamati kwa ajili ya kupitia upya mchoro uliokuwepo na kuandaa utaratibu ili kuanza mchakato ya ujenzi kwa kuwa tayari Rais alishazungumza hivyo unapaswa kutekelezwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mtaka alipongeza juhudi za TBA kwa miradi mbalimbali wanayoisimamia ikiwemo mradi wa ujenzi wa hosteli za wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Mtaka alisema kwa upande wake hakuridhishwa na gharama za mradi huo, kwa kuwa thamani ya mradi haikuendana na thamani ya fedha iliyotajwa.

“Gharama iliyotajwa ni kubwa, niliamua kuwasiliana na viongozi wengine mkoani, lakini nashukuru Rais alikuja na yeye hakuridhishwa na gharama hiyo ndipo alitutaka tuje TBA Dar es Salaam kuangalia miradi pamoja na kufanya mazungumzo ya jinsi ya kutekeleza mradi wa ujenzi wa hospitali kwa gharama ya Sh bilioni 10 ambayo ameahidi kuitoa,” alisema Mtaka.

Aidha, alishauri taasisi za serikali zinazohusika na mambo ya ujenzi kuwa wabunifu na kuifanya nchi kuwa na mfumo wake wa ujenzi ambao utakuwa sio wa kuiga kutoka katika mataifa mengine.

“Tunataka tujenge mkoa mpya wa kiuchumi, hatuwezi kusema tunakwenda kwenye uchumi wa kati wakati hatuna mikoa iliyoandaliwa, tunaamini Rais akituunga mkono kwenye ujenzi wa hospitali yetu na tukathubutu kufanya ujenzi huo tutakuwa tumemsaidia Rais pamoja na kufanya na mikoa mingine ambayo haina hospitali za rufaa kuiga,” alisema Mtaka.

Post a Comment

 
Top