0

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo pamoja na mashahidi wenzake wanne wanatarajia kutoa ushahidi mwezi ujao katika kesi inayomkabili Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) pamoja na na mkewe Neema Lema.

Kwa mujibu wa Wakili wa Serikali, Alice Mtenga, licha ya Gambo pamoja na wenzake wanne kutoa ushahidi wao Februari 3, mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, pia watakuwa na vielelezo vitatu vitakavyotolewa mahakamani hapo.

Mtenga alisema hayo jana mbele ya Hakimu Nestory Barro wakati akiwasomea maelezo ya awali washtakiwa hao ambao ni mume na mke.

Aliwataja mashahidi watano watakaotoa ushahidi wao ni Gambo, Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Arusha (RCO), George Katabazi, ASP Damas Massawe, mhusika kutoka Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom pamoja na mtaalamu wa picha.

Pia alivitaja vielelezo watakavyovitoa katika kesi hiyo kuwa ni nakala ya taarifa za mawasiliano ya simu kutoka Kampuni ya Vodacom, simu ya mshtakiwa ambaye ni mke wa Lema pamoja na ripoti ya uchunguzi kutoka Kitengo kinachoshughulikia masuala ya kiuchunguzi (Forensic Bureau).

Awali akiwasomea maelezo ya kesi hiyo, Wakili Mtenga alidai kuwa Godbless Lema na mke wake Neema, wanashtakiwa kuwa kati ya Agosti 20, mwaka jana ndani ya Jiji la Arusha, walimtumia ujumbe wa simu ya kiganjani mkuu huyo wa mkoa wenye lugha ya matusi huku wakijua ni kosa kisheria.

Alidai ujumbe huo ulitumwa kutoka namba 0764150747 kwenda namba 0766-757575 uliokuwa ukidai, “Karibu, tutakuthibiti kama Uarabuni wanavyothibiti mashoga.”

Baada ya kuwasomea maelezo hayo ya awali, washtakiwa hao kwa pamoja walikiri kuwa ni wakazi wa Arusha na Lema ni Mbunge wa Arusha Mjini ila walikataa kusambaza ujumbe huo wa kumtukana Gambo.

Post a Comment

 
Top