0

KAIMU Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ally Hapi amekitaka Kikosi cha Kupambana na Ujambazi jijini Dar es Salaam kuendelea kuwashughulikia wahalifu kikamilifu ili amani na utulivu viimarishwe nchini.

Hapi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, alisema hayo jana Dar es Salaam katika hafla ya kutunuku nishani, vyeti na zawadi kwa kikosi hicho chenye askari 25, wakiwemo wanawake wanne.

Alisema Jeshi la Polisi kazi yake ni kuhakikisha wananchi wanafanya kazi kwa amani na utulivu, hivyo haiwezekani kikawepo kikundi ama mtu mmoja mwenye uwezo wa kuwakatisha tamaa.

“Endeleeni kuwashughulikia vilivyo, endeleeni kuwasaidia wananchi pia waelewe ni nini haki yao kwa kuwa jeshi la Polisi ni askari waliokula kiapo,” alisema Hapi na kuongeza kuwa raia wema wapo wengi kuliko waovu hivyo haiwezekani hao wachache wakatishe wengine tamaa.

Alikitaka kikosi hicho kuhakikisha kinawakamata raia wanaotembea na silaha barabarani, akitolea mfano kama AK47 na SMG kwa kuwa kwa kufanya hivyo ni kama wanatangaza vita huku kukiwa hakuna duka lolote linalouza silaha hizo, hivyo wakabiliwe.

Awali akizungumza katika hafla hiyo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema kupewa zawadi kwa askari wa kikosi hicho kunahamasisha wengine kufanya vizuri zaidi na wamefanya kazi vizuri kwa mwaka jana.

Mmoja wa askari wa kikosi hicho ambaye ni mwanamke (hakutaka kutaja jina lake), alisema anafurahia nishani hiyo ambayo ni mara ya tatu kupewa ingawaje anatekeleza kazi yenye changamoto mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kujitoa bila kujali linaloweza kutokea mbele yao.

Alisema licha ya kuwa katika kikosi hicho kwa muda, lakini tukio ambalo linampa kumbukumbu zaidi ni lile lililotokea mwaka jana, Septemba 3, eneo la Mikocheni kwenda kupekua nyumba iliyodaiwa kuishi majambazi wakiwemo pia Wakenya.

Alisema katika tukio hilo ambalo walikwenda usiku wa manane, hakujiamini akijua lolote linaweza kujitokeza, lakini yeye na wenzake walikuwa tayari kulikabili.

Post a Comment

 
Top